December 9, 2016




Na Saleh Ally
KLABU ya Azam FC ilianza mapema kuonyesha njia baada ya kuanzishwa kwa kufanya mambo ambayo hakuna ambaye alikuwa hawezi kusema ni mazuri.

Azam FC ilionyesha namna ambavyo timu ya soka inapaswa kuwa, mambo yake yanavyoweza kwenda na kadhalika, na jambo muhimu ilikuwa ni kufuata utaratibu wa mambo yanavyotakiwa.

Mfano, kuwa na uwanja wake wa mazoezi, sehemu maalum ya mazoezi kama gym, bwawa la kuogelea na vifaa bora vya mazoezi.

Unakumbuka kuna wakati fulani niliwahi kusema wachezaji wa Azam FC hawakuwa wakiutendea haki uongozi wa klabu hiyo kwa kuwa wanapata kila kitu na inawezekana kabisa kuwalinganisha na wanavyohudumiwa wale TP Mazembe lakini hawakuwa wakiulipa uongozi wao kwa hali inavyotakiwa.

Kuna wakati niliwahi kuandika kuulalamikia uongozi wa Azam FC kwa kuanza kuonekana unapotea na unatoka kwenye malengo kwa kuwa mambo yake mengi yalikuwa yanaendana na yale ambayo tunayaona hayafai na yamekuwa yakifanywa na klabu kongwe za Yanga na Simba.

Zaidi kilichokuwa kinapeleka tabia hizo mfanano ni kuwa na watu wanaofanya kazi ndani ya Azam FC lakini mapenzi yao yapo Yanga na Simba na tabia zao pia ni za Kiyangayanga pia Kisimbasimba.

Ninaamini kuna mabadiliko baada ya pale na huenda Azam FC wamekuwa wakifanyia kazi katika yale ambayo tumekuwa tukiwashauri kwa kuwa wanagundua kuwa wanaowashauri ni watu wenye nia nje kwao na si kuwakosoa kwa kulenga kuwahimiza.

Leo, lengo kuu la makala ni kuwasisitiza kwamba Azam FC wanachofanya katika suala la kutafuta vijana, ni jambo ambalo Tanzania imelisubiri kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Kusaka, kuinua na kuvikuza vipaji vya Watanzania wadogo kwa umri, mfano tuanze na watoto na baadaye vijana.

Timu ya watalaamu wa soka ya vijana wakiwemo kutoka Uingereza ambao wanasimamiwa na Azam FC wamekuwa wakipita sehemu mbalimbali za nchi yetu Tanzania kusaka makinda ambao wana vipaji na baada ya hapo inawachukua na kuwainua na kuwakuza kwa lengo la kuwaendeleza.

Lengo la Azam FC ni kupata watu sahihi kwa ajili ya mchezo wa soka ambao pamoja na vipaji watakuwa wamelelewa katika mazingira ya mchezo huo na wakati wanakua inakuwa ni rahisi kwao kufuata misingi sahihi kwa kuwa wamefundishwa.

Azam FC inafanya hivyo kwa kuwa ina uhakika pa kuwaweka watoto hao. Inafanya hivyo kwa sababu inataka kuwa na uhakika wa mambo, kuwa na watu sahihi na wakati mwingine nafikiri waliamua kufanya hivyo baada ya kuona vijana wengi wanaowalea kimafunzo ya soka, hawakuwa na msingi mzuri na huenda waliwasumbua.

Kazi wanayofanya Azam FC si ndogo hata kidogo, lakini ukiachana na ugumu ina gharama kubwa. Kwangu ukiniuliza nataka nini, nitakuambia Serikali ya Tanzania kuweka ukaribu na kuwasaidia Azam FC kwa wanachokifanya.

 Serikali inajua ifanyeje kuwapa nguvu na msaada. Huenda wana bajeti yao inajitosheleza, lakini bado kuna nafasi ya serikali kuingia na kuwapa nguvu Azam FC kuhusiana na wanachokifanya.

Lazima tukumbuke wanachokifanya Azam FC kabla hakiwezi kuwa na faida kwao tu. Hata ikiwa ndiyo hivyo lakini lazima suala hilo litakuwa na faida kwa serikali ya Tanzania na watu wake.

Serikali bado haijawa na msaada wa kutoka katika michezo ambayo kweli ni furaha, afya na ajira. Lakini unaweza kusema michezo ni maisha ya watu na haikwepeki, hivyo kwa watu wanaojitolea kama Azam FC, tena kutafuta vijana wazalendo wa Kitanzania, hakika wanapaswa kuigwa na wengine lakini lazima wasaidiwe na serikali ili kuonyesha kuwa wanaofanya vizuri ni wazalendo na wanapaswa kuungwa mkono.

Mwisho niwaase Azam FC kuwa, walichokianzisha ni kitu bora, lakini kinahitaji mwendelezo hadi matunda yatakapopatikana na kuendelea kupatikana.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic