December 2, 2016



Na Saleh Ally
KAMA ambavyo tulianza kuandika kwamba Simba iko katika mazungumzo na kipa wa Medeama ya Ghana, Daniel Agyei.

Simba ilikuwa katika harakati hizo kwa siri ikitaka kumsajili kipa huyo. Mwisho hilo limethibitika baada ya kipa huyo kutua nchini juzi tayari kwa ajili ya kumalizana na Simba.
Uliona mabegi aliyotua nayo Agyei akitokea Ghana, katika akili ya kawaida, jibu lilikuwa ni kwamba hatarudi Ghana kwa kuwa alishaelewana na Simba.

Kama kilichobaki ilikuwa ni kutia saini tu tayari kuanza kazi chini ya Kocha Joseph Omog raia wa Cameroon ambaye imeelezwa kwenye ripoti yake alieleza kwamba anataka beki wa kati, mshambuliaji mmoja na kipa.

Kipa wa nini, unaona kazi nzuri aliyoifanya kipa Vicent Angban ambaye alifanya vema kuliko kipa mwingine yeyote wa Ligi Kuu Bara katika mzunguko wa kwanza na akafungwa mechi mbili za mwisho, yaani Simba ikipoteza mechi mbili za mwisho akiwa langoni.

Ukiangalia mechi hizo, unagundua Angban hakuwa katika kiwango kizuri na alikubali kufungwa kilaini. Ukisema amechoka nitakataa, lakini Simba imeamua kuongeza nguvu ya makipa kwa madai ya kumpa changamoto.

Kama unazungumzia changamoto kwa kumsajili kipa kama Agyei, mimi nitakukatalia na hakika naweza kusema ameletwa Agyei na hakuna ubishi, Angban anakwenda kukaa benchi na kinda mwingine Peter Manyika.



Kila mmoja aliona kazi ya Agyei ambayo hakika haizuii kusema ni moja ya kazi bora kabisa katika mchezo wa soka nchini. Alikuwa katika kiwango bora wakati wa michuano ya Kombe ya Shirikisho la Afrika alitoa msaada mkubwa kwa timu hiyo ya Ghana kufanya vizuri kuliko hata Yanga ya Tanzania.

Agyei anatua, kama hatadaka yeye kwa maana ya kiwango na uzoefu maana yake nafasi inakwenda kwa Angban tena na unategemeaa kuona Watanzania hawa wawili makinda, Manyika na Denis Richard, ndiyo safari imewakuta.

Wakati Manyika angalau alikuwa ana nafasi ya kudaka baada Angban, sasa anasubiri chini baada ya Agyei kuwasili. Hakika unaweza kusema huu ni mwisho wa Manyika na kama anataka kujifunza na akue basi aondoke Simba.

Manyika ana uwezo, Simba hawakumuamini huenda kutokana na makosa kadhaa ya msimu uliopita. Kipaji anacho na yeye ameamua kurejea katika nafasi ya kufanya vema baada ya kuwa amechotwa na utoto.

Wakati anarejea, anakuta makipa wawili wa nje, wenye uwezo kuanzia michuano mbalimbali wakiwa mbele yake na wana nafasi ya kucheza bila yeye. Hakuna cha kubisha hapa kwamba hakuna nafasi ya Manyika kuwa bora kwa kukuza kiwango chake bila ya kucheza.

Kama ni kuutafuta ubora, hata kama Manyika aliamua kuwa ‘siriaz’ ilikuwa ni lazima acheze. Hivyo tukubali, kumleta Agyei ni Simba kumchimbia kaburini Manyika na mwenzake Denis. Ukweli ni ujumbe wa moja kwa moja kwamba kwa sasa hawana nafasi Simba labda hapo baadaye.

Inawezekana kabisa kati ya hao wawili, Manyika na Denis wanapaswa kukubali kwamba walipo sasa si sehemu sahihi kwao. Kama wanapaswa kukuza vipaji vyao basi watafute sehemu ambayo watapata nafasi ya kucheza.

Lazima wacheze ndiyo waendelee kukua. Umeona Denis alikwenda Daraja la Kwanza akawa nyota aliyeipandisha timu daraja, bahati mbaya ikakumbwa na kashfa ya upangaji matokeo.
Kwa Manyika, kwake ulikuwa ndiyo wakati mwafaka wa kucheza na si kukaa benchi. Kuletwa kwa Agyei, Simba imeweka msisitizo na kumfikishia ujumbe kwamba bado haaminiki na kweli hauwezi kusema ataaminika mbele ya makipa hao wawili.

Simkatishi tamaa Manyika au Denis, tabia inajulikana ya timu nyingi, Agyei kwa ubora au hapana lazima atapewe nafasi labda aboronge mwenyewe. Baada ya hapo, bado Angban ana nafasi ya pili. Kwa mechi 20 zinazokuja za mzunguko wa pili na zile za Kombe la FA, bado naiona nafasi ndogo ya Manyika kucheza.


Anahitaji kucheza ili kukua zaidi. Umri unamruhusu hata kama anaipenda Simba, akubali kwenda atakapopata nafasi na siku ikifika akiwa na nafasi ya kucheza, atarudi Simba. Benchi mfululizo, litamzeesha ikiwa akili yake imekaa kibenchibenchi tu. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic