December 10, 2016

MSUVA

Baada ya kiungo mkabaji Mzambia, Justine Zullu ‘Mkata Umeme’ kutua Yanga, huenda ukawa na mafanikio kwa winga, Simon Msuva kutokana na aina yao ya uchezaji ilivyo, kwani wameonyesha kuelewana.


Kiungo huyo mwenye sifa kubwa ya kukaa na mpira na kupiga pasi zenye macho, alitua nchini wiki moja iliyopita kutoka kwao Zambia kwa ajili ya kuichezea timu hiyo inayojiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Zullu amefanya mazoezi ya pamoja na timu hiyo kwa siku sita kwenye Viwanja vya Gymkhana, Posta jijini Dar es Salaam na kuonyesha uwezo mkubwa hasa katika kukaba na kupiga pasi zenye macho.

Katika mazoezi ya timu hiyo ya kimbinu waliyoanza kuyafanya wiki hii, kiungo huyo mwenye umbile kubwa, mara zote amekuwa akipangwa kucheza pamoja na Msuva.
Zullu alionekana akicheza kwa kuelewana na Msuva kwa kumpigia pasi ndefu pembeni na kufika miguuni mwa winga huyo, ambaye alimiliki mpira na kuanza kufukuzana na mabeki au kupiga krosi safi.

Msuva alionekana kunogewa na pasi hizo ndefu ambazo awali zilikuwa zikipigwa na kiungo, Athumani Idd ‘Chuji’ na kuonekana uwanjani muda wote akijitenga pembeni akiwatoroka mabeki akisubiria pasi hizo.

Wachezaji hao, kuna wakati walikuwa wakisogeleana wakipigiana pasi fupi wakiwa wanalishambulia goli la wapinzani wao na Msuva kufanikiwa kutengeneza bao lililotokana na krosi safi aliyoipiga baada ya kupokea pasi ya Zullu. Bao hilo lilifungwa na Donald Ngoma.

Akimzungumzia Zullu, Msuva alisema: “Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo wa kumiliki mpira na kupiga pasi, ninaamini kama tukikaa pamoja tukicheza kwa kuzoeana, tutafanya vitu vingi vizuri.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic