LWANDAMINA |
Mabingwa wa Bara Yanga, kwa mara ya kwanza ikiwa chini ya Kocha George Lwandamina, leo Jumamosi inacheza mechi ya kirafiki na JKU ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mbali ya Lwandamina aliyechukua nafasi ya Hans van Der Pluijm, Yanga pia itacheza kwa mara ya kwanza kikosini ikiwa na kiungo Justine Zullu na kocha msaidizi Noel Rodwell Mwandila.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wamefanya mazoezi kwa wiki mbili na sasa ni wakati wa kutazama kile walichofanya.
“Kikosi kipo vizuri na maandalizi yote ya mechi hii yapo sawa, tunataka kupima kikosi chetu tunaomba mashabiki wetu waje wengi kutazama kikosi chao kipya,” alisema Saleh.
Yanga inacheza mechi hii ikiwa imesaliwa na siku tano za kufanya usajili huku ikielezwa kupanga kutumia mchezo huo kumuaga mchezaji wake kiraka aliyemaliza mkataba Mbuyu Twite.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa JKU, Omar Othman, alisema; “Maandalizi yetu yapo vizuri, watu wategemee upinzani mkali kutoka kwetu hivyo Yanga wajiandae kwa mchezo wa mapambano.”
0 COMMENTS:
Post a Comment