Ikiwezekana unaweza ukasema kuwa ni rekodi mpya imeandikwa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya wachezaji wawili tu wa Yanga kuhusika kwenye mabao matatu ya timu hiyo.
Yanga wikiendi iliyopita ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi uya JKT Ruvu, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lakini wachezaji Haruna Niyonzima na Simon Msuva wameweka rekodi mpya.
Katika mchezo huo, Msuva alionekana amefaidika sana na mfumo wa kocha mpya wa timu hiyo George Lwandamina baada ya kufanikiwa kufunga mabao mawili.
Msuva ambaye amefikisha mabao tisa alifunga mabao hayo kwa pasi zote za Niyonzima, lakini pia wawili hao ndiyo walihusika kwenye bao lingine baada ya Niyonzima kumpa pasi Msuva wakati anataka kufunga mpira ukamgonga beki wa JKT, ambaye alijifunga.
Ukitazama kwa umakini kwenye dakika tisini za mchezo huo utakubali kuwa hawa ni watu hatari sana kwani mbali na kufunga mabao hayo pia walikosa nafasi kadhaa za kufunga huku wakionyesha kuwa na uchu mkubwa kuliko washambuliaji wa timu hiyo.
Baadhi ya mashabiki wa Yanga waliona mabadiliko makubwa kwa wachezaji hao huku kila mara wakiwashangilia, lakini hakika walionyesha kuwa ni wachezaji hatari ambayo wanaweza hata kufunga mabao saba kwenye mchezo mmoja kama mabeki wa timu pinzani hawatakuwa makini.








0 COMMENTS:
Post a Comment