December 2, 2016
Na Saleh Ally
UONGOZI wa Yanga ulianza mazungumzo ya siri na Kocha Mkuu wa Zesco wakati huo, ukamleta hapa nchini kwa siri na kuzungumza naye na baadaye akarejea nchini na kuingia mkataba wa miaka miwili.

Hali hiyo ilimuudhi aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga wakati huo, Hans van der Pluijm raia wa Uholanzi akaamua kuandika barua ya kujiuzulu akiona alikuwa akionyeshwa dharau.

Yanga wakashirikiana na mmoja wa shabiki mkubwa wa klabu hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye anajulikana kwa kupenda michezo, kumshawishi Pluijm abadili uamuzi wake.

Hata hivyo, Yanga haikuacha uamuzi wake wa kumchukua Lwandamina ambaye anaonyesha atakuwa njia ikiwa imelenga kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwa imefanya vema katika Kombe la Shirikisho chini ya Pluijm.

Mwisho, Yanga imekaa mezani na Pluijm na kukubaliana naye kuwa apande cheo na sasa awe ndiye bosi wa Lwandamina maana Pluijm ni mkurugenzi wa ufundi.

Uamuzi wa Yanga unaweza kusema ni mzuri kwa kuwa Lwandamina ameingia kazini, Pluijm amebaki naye anaendelea na kazi. Lakini jiulize kwa nini wote wapo? Ukitulia utaweza kuona hakukuwa na sababu kubwa sana ya wote kubaki.

Pili jiulize, kama Yanga imeongeza nguvu kwa kuajiri kocha mpya, ambaye inamuona ana uwezo wa kuitoa ilipo na kufika mbali zaidi, vipi imembakiza wa zamani?

Kweli Pluijm ni kocha bora, basi kwa nini asingeendelea yeye badala ya Lwandamina. Na kama Lwandamina yupo na ndiyo anaonekana atakuwa msaada, vipi anakuwa tena chini ya Pluijm ambaye ameonekana anahitaji nguvu ya kocha mpya?

Kocha mpya ambaye amekuja kuweka nguvu kwa uongozi na mbinu zake mpya, vipi zinakuwa chini ya kocha wa zamani ambaye ndiye anakuwa bosi?

Kuna maswali mengi sana ya kujiuliza na huenda mchango mzuri wa Pluijm au presha kubwa ya mashabiki kwamba hawakutaka Mholanzi huyo kuondoka, imewafanya Yanga kutoangalia mbali kwamba kunawezekana kukawa na shida.

Hawa wawili, wote ni makocha wa kiwango cha juu, wote wamecheza timu zao za taifa ambazo ni maarufu duniani na kila mmoja anajiamini ana uwezo mkubwa. Unaweza kusema ni makocha wakubwa katika soka la Afrika, sasa ni mafahari wawili katika zizi moja.

Pluijm atafurahia Lwandamina kuyavuka mafanikio yake? Lwandamina atakubali alishindwa mwenyewe kama mambo hayatamuendea vizuri au uwepo wa Pluijm itakuwa ngao yake ya kisingizo?

Kuna kosa naliona na huenda kuna nafasi ya kujifunza mbele kwa kuwa walichokifanya Yanga, huenda kimekaa kisiasa, kirafiki au kupeana moyo kuliko kiufundi zaidi.


Kabla Yanga ilifanya maamuzi sahihi mara mbili hivi, ikimtoa Ernie Brandts akiwa anafanya vizuri lakini ikashikilia msimamo kwa Pluijm naye akafanya vizuri. Ilimtoa Tom Saintfiet na kweli Brandts akafanya vizuri na wote wakati wakitolewa mashabiki hawakutaka.

Wachezaji asilimia 80 walio Yanga, wamesajiliwa na Pluijm. Unajua wanaweza vipi kumuamini kocha huyo kuliko Lwandamina na kama ikitokea kutofautia kidogo kwa wawili hao ambao ni mtu na bosi wake ni rahisi pia kwa wachezaji wengi kuchagua upande fulani.


Kikubwa ni kuomba yasitokee yote niliyofikiria au kuwaza, lakini katika hili, bado naamini Yanga wamejichanganya na uongozi unapaswa kuwa makini sana na kuwa karibu na kikosi ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa mpangilio sahihi kutokana na makubaliano au kinachotakiwa kufanikiwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV