December 2, 2016Klabu ya Stand United ya Shinyanga imesema imechezwa na ‘machale’ ya kuwepo mchezo mchafu unaotaka kuchezwa na beki wao, Joseph Owino ambaye amekuwa akishinikiza apewe barua ya kuachwa, lakini ili kukwepa kesi wamemtaka aje na barua iliyosainiwa na hakimu ndipo wampe barua ya kumuacha ‘release letter’.

Owino hana maelewano mazuri na viongozi wake tangu abaniwe kujiunga na Fanja ya Oman ambayo ilikubaliwa kumchukua lakini ikashindwa kutimiza masharti ya Stand, ikiwemo kutuma kwanza fedha za kumununua kabla ya kupewa barua ya kumuacha lakini wakakataa.

Tangu kipindi hicho, Owino amekuwa kwenye msigano na uongozi wa Stand huku akibembeleza aachwe huru.

Katibu wa Stand, Kennedy Nyangi ameliambia Championi Ijumaa kuwa wamefikia wazo hilo kutokana na ukweli Owino anawadai fedha ya usajili, hivyo kumpa barua ya kumuacha ni njia ya kuwafungulia kesi.

“Siyo yeye tu, wachezaji wote waliosajiliwa msimu huu hakuna ambaye ameishapata fedha za usajili, lakini mwenyewe amezidi kutushinikiza tumpe barua ya kumuacha na kwamba atasamehe kila kitu.


“Tumemweleza kama amedhamiria kweli, basi atuandikie barua iliyosainiwa na hakimu kuthibitisha kwamba anaondoka kiroho safi, siyo tumpe barua halafu kesho atufungulie mashtaka, hilo hatutaki,” alisema Nyangi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV