December 2, 2016Mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe amesema kuwa katika muda mfupi aliofanya mazoezi chini ya kocha mpya wa timu hiyo, George Lwandamina, anaamini kuwa watafanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Tambwe ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa chini ya Kocha Hans van Der Pluijm aliyebadilishiwa majukumu klabu hapo na kuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, amedai kuwa kuna mambo ambayo tayari ameshayapata kutoka kwa Lwandamina ndani ya muda huo mfupi aliofundishwa naye.

Tambwe amesema kutokana na hali hiyo, anaamini kuwa watafanya vizuri zaidi katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Desemba 17 na kurudi juu katika msimamo wa ligi hiyo.

“Kocha yupo vizuri kwani ni mtu aliye makini na kazi yake, jambo ambalo ndiyo silaha kubwa kwa yeyote kama ilivyokuwa pia kwa Pluijm.

“Tangu alipoanza kukinoa kikosi chetu, kuna mambo ambayo tayari nimeshayapata kutoka kwake, hivyo ni matumaini yangu kuwa nitaendelea kufanya vizuri kwa ajili ya mafanikio yangu pamoja na timu,” alisema Tambwe.


Hata hivyo alipotakiwa kuweka wazi mambo hayo ambayo tayari ameyapata kutoka kwa Lwandamina ndani ya muda huo mfupi, alisema: “Hiyo ni siri yangu sasa ila tambua hivyo.” 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV