December 5, 2016




Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita, mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Samatta alifanikiwa kufunga mabao mawili wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Waasland-Beveren.

Samatta alifunga mabao hayo kwa mara nyingine ikiwa ni siku kadhaa baada ya kukaukiwa mabao ya kufunga huku washambuliaji wengi wakiendelea kufanya vizuri.

Kwa hali ilivyo, inaonyesha wazi kwamba Samatta amekwenda kwenye timu yenye ushindani mkubwa wa namba. Kwamba wachezaji anaochuana nao ili kupata nafasi, wako vizuri na lazima ajipange kwelikweli, kufanya vema.

Wote tunamjua Samatta, ni mtu mwenye nia, malengo na anayetaka kutimiza ndoto zake. Kwani mimi na wewe kama si wazazi wake au watu wachache wa karibu yake, hakuna anayeweza kutamba kwamba alikuwa msaada mkubwa kwake.

Samatta sasa ndiye nyota ya nchi yetu kama utazungumzia mchezo wa soka. Ndiye mfano na mtu ambaye anaweza kuwatamanisha wengine kupata mafanikio makubwa kisoka.

Nimeamua kuandika makala baada ya kupitia mijadala mtandaoni, kukutana na watu kadhaa na kukaa katika kundi moja na wapenda mpira fulani ambao walikuwa wakijadili na kuonyesha Samatta amewahi kuondoka Mazembe na wengine wakisema Genk haikuwa chaguo sahihi.

Kauli kama hizo ni ukatishaji tamaa wa hali ya juu, hauna sababu za msingi kuwekwa mbele kama sehemu ya uendeshaji wa jambo ambalo linahitaji uhamasishaji wa mambo mema kwa ajili ya kutengeneza njia bora inayoweza kuzalisha watu bora na wanaoweza kuitwa mfano.

Kutoa maoni, si rahisi kumzuia kila mmoja lakini kwa kila kinachozungumzwa, lazima tukubali kwamba Samatta naye ni mtu na anahitaji mambo mengi sana ya kushinda katika maisha.

Ulaya ni mazingira tofauti na DR Congo, lakini hata mfumo wa kila kitu unapishana na sasa hata nusu msimu bado. Samatta ameonyesha uwezo mkubwa kabisa na hakuna anayeweza kuwa na hofu naye katika suala la ufungaji.

Watanzania tuliungana kumzodoa na kumsema Hasheem Thabeet kwamba amefeli, ni mtu wa starehe, anajiona na kadhalika na ndiyo maana ameshuka hadi kushindwa kuendelea kucheza kwenye Ligi ya Mpira wa Kikapu (NBA).

Wakati wa mjadala wa kukosa, wengi walijitokeza na kuchangia, kila mmoja alikuwa mwalimu na ana lake ilimradi kunapofikia kulaumu, kila mmoja anaweza kuwa na “mdomo mkubwa” kuzidi “kichwa” chake. Hasheem alipofanikiwa na kufikia kucheza NBA, waliopongeza hawakufikia hata robo ya wale waliokosoa.

Kitu kibaya zaidi waliokosoa, wengi hawakuwa na uhakika wa robo ya maneno waliyosema kama hiyo Hasheem ni mtu wa starehe sana au vyovyote vile. Wengi wakazungumza maneno ya kukatisha tamaa na ya kushangaza kabisa.

Mimi ninaamini hivi; hata kama umri wake unakwenda, siku itafika na Hasheem atarejea na kucheza NBA. Mimi nabaki kwenye kundi la wale wanaompa moyo na kumshauri asikate tamaa na siku moja arejee tena NBA na kuwashangaza waliokuwa wakishambulia bila ya kuangalia uhalisia, kupima wanachokisema au kuangalia uhakika wa wanachokitoa kwenye ndimi zao.

Sasa ile ya Hasheem, tusimtwike mapema Samatta. Kama ikionekana hana mwendo mzuri, basi tusiibuke na maneno ya kumkatisha tamaa kama yale aliyotwikwa Hasheem na wasemaji wakaonekana hawana uhakika hata chembe.

Kukosea kupo, kukosea kunaweza kuwa darasa bora kabisa kwa wenye uwezo wa kukosea na kujirekebisha. Samatta amefika mbali lakini hajamaliza na tukubaliane anahitaji kwa ukubwa wa juu kabisa kupewa moyo na kuungwa mkono.


Tunajua mfumo wa michezo hapa nyumbani ni pumba tupu, viongozi wake ni ovyo na serikali haina habari hata kidogo. Basi kwa hao wanaokuwa wamejitahidi na kutoka, tuwaunge mkono na kuwapa moyo hata kama kweli tutakuwa tunawakosoa.

1 COMMENTS:

  1. kuna tofauti kubwa kati ya samata na hasheem na nyie waandishi kuficha ukweli ndio tatizo kubwa na hamuwasaidii wanamichezo,ni ukweli usiopingiks kuwa life style ya maisha ya hasheem ilichangia sana kushuka kiwango,ligi ikisimama anarudi nyumbani kutanua na starehe wakati hata wachezaji wenye majina makubwa kama kobe huwa wanakodisha wakufunzi maalumu ili kuwanoa,hivi unafahamu kuwa kobe huwa anaendelea na mazoezi binafsi kwa masaa mawili kila baada ya mechi,unaweza ukawa unajua zaidi soka ila nadhani hujui basketball,hasheem wakati anaondoka alikuwa ni mchezaji wa tatu toka chini katika viwango vya wachezaji wote wa NBA huku akiwa ni mchezaji mrefu kuliko wote katika NBA,mbwana anaweza kufika mbali kwani hata style ya maisha yake ni tofauti sana na hasheem ana nidhamu na kufuata miiko ya michezo,huwezi kumsikia kampiga trafiki au TID(mfano} ma unajua makosa kama hayo kwa NBA ni ishu kubwa sana hata kama yamefanyika nje ya uwanja, bahati nzuri hawana connection na kinachoendelea bongo,kama unataka kumsaidia hasheem na unampenda kweli basi muambieni ukweli sio kumtetea kwa makosa ya kijinga,

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic