January 2, 2017


Kikosi cha Azam FC ambacho leo Jumatatu kitaanza kutupa karata yake ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi dhidi ya Zimamoto, kinatarajiwa kukosa huduma za nyota wake watano wa kikosi cha kwanza wenye matatizo mbalimbali.

Nyota hao ni Joseph Mahundi na Hamis Mcha ambao ni majeruhi, Mghana, Daniel Amoah na Himid Mao wakiwa na matatizo ya kifamilia pamoja na nahodha John Bocco ambaye alichelewa kujiunga na wenzake baada ya kutakiwa kuhudhuria kliniki kutokana na matatizo ya meno yanayomsumbua.

Meneja wa Azam FC, Phillip Alando, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, hao pekee ndiyo wana asilimia kubwa ya kutokuwepo, lakini kikosi chao kipo kamili kwa mchezo wa leo huku matarajio yao yakiwa ni kuanza vema.

“Kikosi kipo kamili lakini tunatarajia kuwakosa nyota wetu kama watano hivi wenye matatizo mbalimbali. Nahodha John Bocco tulimuacha Dar kwa kuwa alitakiwa kuhudhuria kliniki kutokana na matatizo ya meno yanayomsumbua.

“Mahundi na Mcha ni majeruhi, Amoah yupo kwao Ghana akishughulikia matatizo ya kifamilia kama ilivyo kwa Himid ambaye kesho (leo Jumatatu) anatarajia kuungana na sisi.

“Kwa ufupi, kocha wetu Idd Cheche amesema hatafanya mabadiliko sana kwenye kikosi na anaamini vijana wake wataibuka na ushindi katika mchezo wetu huu wa kwanza,” alisema Alando.


Katika michuano hiyo, Azam imepangwa Kundi B sambamba na Yanga, Zimamoto na Jamhuri. Azam itaanza kutupa karata yake leo saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Amaan visiwani humo, kabla ya saa 2:30 usiku Yanga kupambana na Jamhuri, uwanjani hapo.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic