January 2, 2017Mabingwa wa Tanzania Bara cha Yanga, leo usiku kinashuka uwanjani kupambana na Jamhuri ya Pemba katika mchezo wake wa kwanza wa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea kutimua vumbi Visiwani Zanzibar katika Uwanja wa Amaan ulipo mjini Unguja.

Katika mchezo huo, Yanga imepanga kutumia majembe yake yote ili iweze kuibuka na ushindi utakaoiwezesha kukaa kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo ambayo inashirikisha timu tisa.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, amesema kuwa wamejipanga vilivyo kwa ajili ya mchezo huo kuhakikisha wanapata ushindi mnono ili waweze kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Alisema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, wanatarajia kutumia kikosi chao kilekile ambacho wamekuwa wakikitumia katika michuano ya Ligi Kuu Bara.

“Tupo visiwani hapa kwa kazi moja tu ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote, hatuangalii timu tutakayokutana nayo, iwe Simba au Azam sisi tutaingia uwanjani kuhakikisha tunapata matokeo na tutakuwa tukipanga kikosi cha ushindi.

“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo, wachezaji wote wapo vizuri, hatuna majeruhi hata mmoja, hivyo tunamshukuru Mungu kwa hilo,” alisema Mwambusi.


Yanga ipo Kundi B katika michuano hiyo na timu za Jamhuri, Azam na Zimamoto wakati Kundi A lina timu za Simba, Taifa Jang’ombe, Jang’ombe Boys, KVZ pamoja na URA ya Uganda ambayo ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambayo hufanyika kila mwaka visiwani humo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV