January 6, 2017





Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita, niliandika kuhusiana na waandaaji wa Kombe la Mapinduzi kuboresha mashindano yao ambayo naweza kusema sasa umaarufu umekuwa ukizidi kupanda.

Nilieleza namna ambavyo ninaamini kwamba mashindano hayo yangeweza kupiga hatua zaidi na ikiwezekana hadi kuyafunika yale ya Afrika Mashariki na Kati kwa klabu, maarufu kama Kombe la Kagame.

Ushauri wangu ulisisitiza waandaaji kuacha kujificha katika kivuli cha siasa kwa kuwa ni mashindano ya Mapinduzi, basi kila kitu kiende ilimradi tu.

Mwisho nilieleza lazima waandaaji wajue kwamba timu pia zina gharama kubwa. Hivyo waheshimu hilo lakini pia kujua hadhi ya timu zinazoshiriki hata kama ushiriki wao unalenga kuboresha umoja wa nchi yetu, hasa muungano wa Zanzibar na Tanganyika, pia majirani zetu kama Uganda au Kenya.

Pamoja na hivyo, lazima timu ziende katika mashindano ambayo zinaona yatakuwa na faida kwao. Klabu inaendesha timu kibiashara, hakuna ubishi ukisema biashara, kitu muhimu zaidi ni faida.

Nilishauri kuhusiana na zawadi za bingwa, iboreshwe na nyingine pia kama mfungaji bora na kadhalika ili kuongeza chachu ya ushindani itakayosaidia mashindano kuimarika kiushindani na kuongeza mvuto zaidi.

Wakati michuano inaendelea, hakika inaonekana inavutia na ina ushindani. Niwapongeze waandaaji. Pia naona hadi sasa, waamuzi wanaonekana kujitahidi na huenda malalamiko hayatakuwa mengi sana, ambalo ni jambo bora kabisa.

Kuna jambo nimeliona, hili ningependa niwakumbushe waandaaji kwamba haliendani na hadhi ya mashindano yao na hakika linavyofanyika huenda ni jambo la karne iliyopita. Kwangu naona kama waandaaji hawaijui thamani ya mashindano yao ilipofikia.

Kila baada ya mechi, mchezaji bora na manahodha wa timu zote mbili, wanasogea pale pembeni ya uwanja na kugawiwa juisi ambazo ninaamini hutolewa na mmoja wa wadhamini wa mashindano hayo, Kampuni ya Azam.

Kwanza niwapongeze Azam kujitokeza kudhamini na pia kutoa zawadi hiyo. Kwangu nasema hakika tunaonyesha kiasi gani tumechelewa, tumekubali kuchelewa na tumeridhika kuendelea kuchelewa bila kuchoka!

Hivi kwa mashindano kama hayo ambayo sasa yanajulikana ni kama ya kimataifa, kweli ni sahihi mchezaji aliyeonyesha soka la kuvutia mwisho wa mchezo akapewa katoni za juisi?

Inawezekana waandaaji waliona sawa na lilikuwa ni wazo la wadhamini. Wakati mwingine umakini wa mwandaaji unaweza kumsaidia mdhamini kujitangaza zaidi na akajitangaza kwa njia iliyo sahihi kuliko ile ambayo inashindwa kutofautisha michuano kama hiyo iliyofikia hatua ya kuitwa ya kimataifa na ile ya ndondo.

Uonyeshe soka vizuri, halafu ukanywe juisi au upewe katoni ya juisi, kweli ni sawa? Tena anapokabidhiwa mchezaji ni sehemu inaonekana ni kama vile sokoni na hakuna maandalizi yoyote yanayoonyesha ni sehemu maalum kwa michuano mikubwa kama hiyo.

Hata bango tu la bidhaa za mdhamini nyuma ya sehemu makabidhiano yanapofanyika, lingekuwa msaada mkubwa sana.

Kuliko kukabidhi katoni za shilingi laki moja au mbili, bora kingetengenezwa kikombe kidogo mfano wa chupa ya juisi ambacho angekabidhiwa mchezaji kikiwa kimeandikwa jina la hiyo juisi au soda na mchezaji angekaa nacho siku nyingi huku mdhamini akijitangaza.

Kuzigawa juisi bure zinamsaidiaje mdhamini kujitangaza bure? Kibiashara pia si jambo zuri. Kwa waandaaji kwa maana ya hadhi ya mashindano, pia si jambo zuri na huenda litaonyesha ni mashindano yasiyo na lengo la kuendelea kukua na kufika mbali.

Wanaoandaa lazima niwapongeze kwamba wanajitahidi, ndiyo maana yapo hapo. Kama ninaona wanakosea, siwezi kuwafumbia macho, badala yake kama hilo la kugawa juisi, nasisitiza naona si sahihi hata kidogo.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic