January 6, 2017



Kocha wa Simba, Joseph Omog, jana usiku alionyesha kuwa yeye ni mtu wa maamuzi magumu baada ya kuwaweka nje wachezaji wake muhimu kwenye mchezo mgumu wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA.

Simba walitarajiwa kuanzia kikosi imara kwa kuwa URA ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo na wapo nao moja kundi moja la A, lakini kama vile kocha huyo aliwazuga Waganda hao alifanya mabadiliko kwenye sehemu muhimu katika kikosi chake na kutoka suluhu na URA kwenye Uwanja wa Amaan.

Wakati URA walikuwa wakiingia kwenye michezo yote iliyopita kuwasoma Simba, jana Omog aliwaonyesha kuwa yeye ni kocha kiboko baada ya kumweka nje kipa namba moja wa timu hiyo, Daniel Agyei, akamweka pia nje kiungo wake mahiri James Kotei.

Badala ya wachezaji hao Simba iliwaanzisha kipa Peter Manyika ambaye hakuwa amecheza mchezo wowote kwenye michuano hiyo au kwenye Ligi Kuu Bara hivi karibuni.

Lakini pia kocha huyo alimuanzisha kwa mara ya mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Laudit Mavugo.

Mabadiliko haya yalionyesha kuwachanganya URA, ambao waliingia wakiwa wanapania kupata ushindi kwani ni sahihi kwamba mbinu zao zilivurugwa.

Mbali na kuwaanzisha hawa kocha huyo pia alimuingiza kwa mara ya kwanza Hija Ugando ambaye alichukua nafasi ya Shiza Kichuya dakika chache kabla mpira haujamalizika.

Hata hivyo, wachezaji wote hao walionyesha kiwango cha juu na kuwasaidia Simba kufikisha pointi saba ambazo zimeendelea kuwaweka kileleni kwenye kundi lao.

Manyika alionekana kuwa imara zaidi kwani aliokoa michomo mitatu mikali ambayo ingeweza kuleta madhara langoni mwao.

Jambo lingine ambalo Omog alilifanya ni kupunguza viungo wengi na kuwaanzisha washambuliaji watatu, Juma Liuzio, Mavugo na Pastory Athanas ambao hata hivyo walishindwa kuipenya ngome ya Waganda hao.

Hata hivyo, dakika chache pia kabla mchezo haujamalizika, Omog alimuingiza Jamal Mnyate ambaye alikwenda kuchukua nafasi ya Mavugo.

Hii ni sare ya kwanza kwa Simba kwenye michuano hii baada ya kushinda kwenye michezo yake yote miwili.

Kwa mara nyingine timu hiyo ilitoa mchezaji bora wa mechi baada ya Jonas Mkude kuibuka kidedea na kupewa katoni kadhaa za Malta.


Simba sasa watamaliza mchezo wao na Jang’ombe Boys, keshokutwa Jumapili lakini wakiwa na nafasi kubwa zaidi ya kuongoza kwenye kundi kwani wakishinda mchezo wa mwisho watakuwa na pointi kumi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye kundi lao.

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic