January 6, 2017




Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema bila ya woga kuwa kikosi cha Manchester United sasa kimekamata kasi na taratibu wachezaji wengi wanaanza kuelewa Kocha Jose Mourinho anataka nini.

‘Chemistry’ ya Mourinho inaanza kushika kasi, kwamba wachezaji wanaelewa na hii inatoa mwanya kwa kikosi hicho kuwa na nafasi ya kuingia kwenye nafasi nne za juu mwishoni mwa msimu.

Ingawa wengi wamekuwa wakiibeza Manchester United kama timu ambayo haina nafasi nzuri lakini inavyokwenda sasa, baada ya mechi sita huenda ikawa imevuka na kuingia ndani ya nne bora.

Baada ya mechi 20, Man United sasa iko katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 39, Arsenal nafasi ya tano na pointi 41, inafuatia Man City na pointi 42 kama ilivyo kwa Tottenham katika nafasi ya tatu baada ya juzi kuibutua Chelsea kwa mabao 2-0.

Ukiangalia hapa, timu zote hizo zimening’inia karibu kabisa na Man United ambayo inakwenda kwa mwendo wa juu zaidi kuliko timu nyingine.

Ushahidi wa hilo uko hivi; katika mechi sita zilizopita Man United imeshinda zote. Arsenal imeshinda tatu, sare moja na kupoteza mbili, Man City imepoteza mbili na kushinda nne, Tottenham imeshinda tano na kupoteza moja.


Mechi dhidi ya Liverpool, itakuwa ni mtihani sahihi kuamua Man United ikae wapi. Kama itashinda, hatari kubwa kwa Arsenal na Man City kwa kuwa kuna kila sababu ya Man United kuwafikia.

Kigezo kingine kinaonyesha Man United kutokana na mfumo wa Mourinho, vigumu kufungwa mabao mengi ambalo ni jambo linalotengeneza uimara wa timu. Katika mechi 20, imefungwa mabao 19, Arsenal na Man City kila moja imefungwa 22 na Tottenham sasa ndiyo ina safu ngumu ya ulinzi ikiwa imefungwa mabao 14 tu.

Angalia katika mechi zake sita zilizopita, Man United imefungwa mabao matatu tu huku ikiwa imefunga 12. Hii inakuonyesha kuwa kuna kitu kimebadilika na kama haitapoteza mechi yake ya saba, basi kuizuia kuingia ndani ya Top Four itakuwa vigumu.

Mwendo wa United unaonyesha namna hali ya kujiamini ya kikosi hicho inavyozidi kuimarika ambalo ni jambo linaloweza kuongeza morali na kuwafanya wachezaji kutamani mafanikio hasa ikizingatiwa ina kikosi chenye wachezaji wengi waliowahi kutwaa makombe wakiwa Man United au katika timu nyingine.

Mwendo wa Arsenal na Man City, kidogo umekuwa hauna uhakika na wakati mwingine ni wa kuyumba. Hivyo hofu inakuwa kuu zaidi kuliko Man United inayozidi kuongeza hali ya kujiamini na kupanda kwa morali.


Mechi dhidi ya Liverpool itakuwa mwamuzi mkuu kwa Man United, kwamba wakati wa kurejea kwenye nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi kuu ‘Top Four’ umewadia. Kama itashindwa, bado nafasi yake haitakuwa imetoweka, badala yake inawezekana kabisa lakini itakuwa imechelewa.

Lakini kama itaifunga Liverpool, Arsenal na Man City zitakuwa timu za kwanza kukaa mkao wa kula na kuipisha Man United kurejea ndani ya Top Four.

MATOKEO MECHI 6 ZILIZOPITA
West Ham 0 -2 Man United
Man United 2- 1 Middlesbrough
Man United 3 -1 Sunderland
West Bromwich 0- 2 Man United
Crystal Palace 1- 2 Man United
Man United 1- 0 Tottenham


MECHI 6 ZIJAZO ZA MAN UNITED
Man United vs Liverpool
Stoke vs  Man United
Man United vs Hull City
Leicester City vs Man United
Man United vs Watford

Man United vs Man City

1 COMMENTS:

  1. yani wewe ndugu yetu unatusomesha vitu ambavyo havipo .man united wamefika nafasi hiyo kwa kubebwa na marefa. ikiwa timu zetu hapa mngesema sana. haiwezekani marefa wakakosea mechi tano zote zilizopita. hawa man united ukiwashambulia tu refa anaanza kazi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic