January 13, 2017Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wenye fedha zaidi barani Afrika wametangazwa huku Mnigeria, Aliko Dangote akiendelea kushikilia namba moja akiwa na utajiri wa dola bilioni 12.1 (zaidi ya Sh trilioni 26).

Jumla ya fedha za mabilionea hao 21 ni dola bilioni 70 (Sh trilioni 152), huku wakipungua mabilionea wawili kwa kuwa mwaka 2015 kulikuwa na mabilionea 23 kukiwa na jumla ya dola bilioni 79.8.
Dangote anaonekana ameporomoka kwa dola bilioni 5 (Sh trilioni 11).

Bilionea namba moja wa Tanzania, Mohammed Dewji yeye anaonekana utajiri wake umepanda kwa dola bilioni 700 na ameendelea kuibeba Tanzania kuwa katika namba 17 katika mabilionea wa Afrika.
 

Pamoja na kuwa katika nafasi ya 17 Afrika, Dewji maarufu kama Mo, amechukua nafasi ya kuwa bilionea kijana zaidi katika Bara la Afrika akiwa na utajiri wa dola bilioni 1.4 (zaidi ya Sh trilioni 3) huku akiwa na umri wa miaka 41 tu.

Mo Dewji ndiye amekuwa tajiri wa kwanza nchini kujitokeza na kusema yuko tayari kuwekeza kwa Sh bilioni 20 ili kununua asilimia 51 za hisa katika klabu maarufu nchini ya Simba.
Simba wamekuwa katika mchakato wa kuhakikisha kila kitu kinakwenda katika utaratibu ili Mo Dewji anunue hisa hizo kwa asilimia 51. Ingawa kuna baadhi ya wazee wa Simba wamekuwa wakionyesha kupinga hilo, jambo ambalo linapingwa zaidi na wengi wao wanaotaka mabadiliko.

Wazee wakiongozwa na Hamisi Kilomoni wamekuwa wakipinga ingawa wengi wao wamekuwa wakifanya mambo yao chinichini kwa kuwa hawataki jambo hilo, ingawa hawajawahi kuweka mezani sababu za msingi huku wakijificha ikionyesha wanajua wanachofanya si sahihi.


Dewji ni Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya MeTL Group ambayo yanafanya biashara zake nchini. Mbali na nyumbani Tanzania, MeTL imekuwa ikifanya biashara zake katika nchini nyingine za Afrika kama Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda na Uganda.

Moja ya malengo makubwa ya MeTL ilitangaza ni kuungana na Rais John Pombe Magufuli katika suala la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ikiwa ni pamoja na uongezaji wa ajira katika sekta mbalimbali kwa Watanzania.
 Kupitia Jarida la Forbes, Mo Dewji alisema:
 “Nimepanga kuwekeza zaidi ya dola milioni 500 (zaidi ya Sh trilioni moja) katika miaka minne ijayo ambayo itaniwezesha kuajiri watu wengine 100,000 zaidi katika ukanda wa Afrika ifikapo mwaka 2021.”

MeTL Group chini ya Mo Dewji inafanya biashara zake zaidi katika masuala ya kilimo, viwanda, mafuta, biashara ya upangishaji majumba, usafirishaji na kadhalika.


Hadi sasa, Kampuni ya  MeTL Group imeajiri wafanyakazi wapatao 28,000 ikiwa ni asilimia mbili ya waajiriwa wote katika sekta binafsi nchini. Hii inamfanya Dewji kuwa mwajiri mkubwa au aliyeajiri wafanyakazi wengi zaidi Tanzania kuliko mwingine.

Hivi karibuni, MeTL Group ilitangaza kuwa imelenga mambo matatu makubwa ambayo ni kutanua mtaji wake zaidi, kujitanua zaidi barani Afrika na kuboresha ubora wa bidhaa zake kwa kiwango cha juu zaidi ya sasa.

Kuendelea kupaa kwa Dewji katika Bara la Afrika kunaonyesha kuwa ni mtu mwenye malengo ya kufanya vizuri, ndiyo maana amekuwa akitaka kuwekeza katika michezo na hasa soka.Dewji ambaye amekuwa ni shabiki na mwanachama wa Simba ambaye alishiriki kwa asilimia kubwa kuisaidia Simba kuing’oa na kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek mwaka 2003, ameendelea kuwa gumzo katika mitandao mbalimbali ya kibiashara kutokana na utajiri wake huo katika umri mdogo.

Katika listi ya matajiri hao, kuna Isabel dos Santos, mwanamama mwenye watoto watatu, tajiri namba moja nchini Angola mwenye umri wa miaka 43. Huyu pekee angalau anaweza kuwa na tofauti ndogo ya umri ukilinganisha na Dewji. Wengi umri wao unaanzia miaka 50 kwenda 60 na zaidi. Hii ni sehemu ya kuonyesha kama ataendelea kukomaa, Dewji anaweza kujijenga zaidi na kama akipata nafasi katika michezo anaweza kufanya vizuri zaidi. Hasa kuigeuza ni faida na pia kusaidia kutengeneza ajira ya juu zaidi pamoja na kutengeneza ajira kwa wingi.1 COMMENTS:

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV