January 13, 2017



Na Saleh Ally
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amekuwa kati ya mawaziri katika Serikali ya John Pombe Magufuli wanaofanya kazi yao kwa ufasaha.


Nape ameonyesha kweli ana nia ya kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo na sanaa, sekta ambayo hakuna anayeweza kukataa hata kidogo kwamba anajitahidi.


Kumpongeza ndiyo kwa kuwa ameonyesha mwanzo mzuri katika mwaka wake mmoja wa uongozi. Ameshirikiana na kila upande, ukizungumzia michezo na kwenye sanaa.


Katika michezo ameonyesha si mtu wa upande mmoja hasa kama ni suala soka pekee, badala yake amekwenda kwenye michezo mingine mbalimbali na kusaidia kadiri anavyoweza.
Amesaidia wanariadha kupata mikataba ya kuwasaidia kuwaandaa kwa ajili ya kuliwakilisha taifa na kadhalika.

Amesaidia masuala kadhaa yanayohusiana na soka.
Tunajua hata katika sehemu ambayo lilitakiwa suala la kukemea, basi Nape hakuwa muoga, hakujali siasa za michezo au siasa za soka au zile za Yanga na Simba na badala yake alikuwa mkweli akionyesha ni kiongozi anayetaka kubadilisha mambo.

Kwenye sanaa, ameshirikiana kwa ukaribu wa hali ya juu na wasanii wa nyanja mbalimbali. Ushiriki wake umekuwa ni wa vitendo na watu wa Bongo Movie na Bongo Fleva wanaweza kuwa shahidi katika hili.

Si rahisi afanye kila kitu kwa mwaka mmoja, haitakuwa rahisi kumfikia kila mmoja kwa wakati huo. Wako alioshirikiana nao na wako aliowafikia na wanaweza kuzungumzia msaada wake.

Kama kiongozi anashiriki hadi kuhakikisha wasanii wanapata bajeti ya kurekodi video bora, wakati mwingine kusafiri kwenda kutimiza ndoto au matakwa yao ya kufanya jambo nje ya nchi. Hakika ni mtu aliyelenga kufanya jambo jema.

Juzi msanii Nasibu Abdul ‘Diamond’, amemshukuru Nape kwa kujitolea kuishawishi Multichoice Tanzania kuwalipia nauli wacheza shoo wake ambao anaongozana nao kwenda Gabon katika ufunguzi wa michuano ya Afcon. Kweli Waziri Nape amefanikiwa na kampuni hiyo imejitokeza kuwasaidia. Hili ni moja ya jambo linaloonyesha kuwa ni waziri mwenye lengo la kufanya jambo.

Ninaamini kwa niaba ya serikali, Nape atakuwa na plani ya muda mfupi na muda mrefu. Atakuwa ni mtu anayetaka kufikia mambo fulani ambayo yanahitaji muda kama sehemu ya mafanikio.

Mafanikio yatakayopatikana hayawezi kuwa ya Nape pekee, hayawezi kuwa ni ya serikali pekee. Badala yake yatakuwa ya Watanzania wote ikiwezekana hata wale wasio wasanii wala wanamichezo.

Ndiyo maana nimeamua kukumbusha, kwamba mtu huyu yaani Waziri Nape anapaswa kuungwa mkono na kila upande ambao unaona juhudi zake.

Wasanii wanaweza kumuunga mkono Nape kwa kutambua kuna mtu anatamani mafanikio, hivyo nao wajitume na isitokee ikawa wengi wanategemea msaada wake wakati wao wamelala na hawajitumi kwa jambo lolote kwa kuwa wanajua yupo na atawasaidia kwa kuwa ni waziri na hilo ni jukumu lake.

Pia, wanamichezo nao wajitume wakijua kuna sapoti yake. Upande wa viongozi nao wangebadilika wakaanza kuona aibu au haya kwamba hata waziri naye anaonyesha juhudi kubwa lakini wao wamekuwa chanzo kikuu cha kuanguka katika michezo.

Viongozi wa michezo ndiyo tatizo kubwa la kudorora kwa michezo nchini huku wachache sana wakiwa wamejitolea kuonyesha njia. Soka, ngumi, riadha na hata mpira wa kikapu, viongozi wengi wamekuwa shimo la kuididimiza michezo zaidi.

Sasa mmepata kiongozi mwenye lengo la kuleta mabadiliko. Acheni longolongo, acheni chuki, fitna na ufujaji wa fedha kwa faida ya matumbo yenu, badala yake angalieni kwa ajili ya taifa letu.


Mshikeni huyu Nape mkono, mmepata mtu mwenye hamu ya kusaidia na kubadilisha. Mkiendelea kumuacha aende peke yake, mwisho atachoka halafu michezo na sanaa ilipo, itaendelea kukwama. Kumbukeni, huyu Nape naye ni binadamu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic