January 2, 2017





NA SALEH ALLY
MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi imeanza Desemba 30, 2016, itaendelea hadi Januari 13, 2017 itakapofikia tamati katika visiwa vya Zanzibar. 

Washiriki ni timu kutoka Tanzania Visiwani ambao ni wenyeji, Bara pia nje ya Tanzania.

Michuano hiyo imekuwa ikishirikisha timu kutoka Kenya wakati mwingine Uganda ikiwa ni sehemu ya kuongeza utamu wa ushindani wakati ikifanyika na ikiwezekana kuvutia watu wengi zaidi.

Kawaida kwa kila unayemuuliza atakuambia Mapinduzi Cup ni michuano kwa ajili ya kuboresha undugu na kuonyesha thamani ya siku ya Mapinduzi ambayo iliwakomboa Wazanzibari. Nafikiri ni jambo jema kwa kuwa michezo ni sehemu ya kuongeza ukaribu, undugu na urafiki wa wanadamu.

Rwanda waliutumia mchezo wa soka kwa kiasi kikubwa kurudisha ukaribu, umoja na amani miongoni mwa Wanyarwanda baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994. Hivyo nakubali michezo inaweza kutumika kama ambavyo nimeeleza.

Ingekuwa si michuano ya Mapinduzi, ninaamini huenda Yanga na Simba au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lingeweza kuleta pingamizi kwamba ni vigumu timu kushiriki. Ndani yake kunaweza kukawa na sababu za kisiasa zinazowafanya hata wenye hoja washindwe kusema au kuona haya kwa kuwa wanajua wakihoji, wataambiwa wanawabagua Wazanzibari.

TFF wangeweza kulalamika wakati wa ufanyikaji wa mashindano hayo. Umewahi kuona wapi ligi inasimama wiki mbili, michuano mingine ifanyike? Kawaida ligi inasimamishwa na mechi za kimataifa za timu za taifa au mapumziko kusubiri raundi ya pili. Huu ndiyo ukweli.

Yanga na Simba wanafaidika nini, au timu zinazokwenda kushiriki zinafaidika nini? Kushiriki kwa ajili ya umoja wa nchi ni jambo jema kabisa. Pamoja na hivyo, tukubali kwamba timu zinafanya biashara na kujiendesha zinatumia fedha nyingi sana. Kimahesabu, biashara unapofanya unalenga faida, ukiifanya ukalenga kujitolea ni kujitekenya na kucheka mwenyewe.

Lazima tukubali kuwa wazi na wakweli, kwamba hata kama ni suala la umoja wetu, mfano Tanzania Bara ingekuwepo michuano ya Uhuru, basi waandaaji watafute wadhamini kwa nguvu, Serikali ya Zanzibar nayo iwasaidie pia ili mambo mengi katika michuano hiyo yaboreshwe na iachwe kupelekwa kwa hisia tu na badala yake kwa kufuata hali halisi ya mambo.

Sasa zawadi ilikuwa Sh milioni 10 kwa bingwa. Ninaamini ni mshahara wa wachezaji wawili tu Yanga au watatu wa Simba. Angalia, wachezaji wanaopigania ubingwa wa Sh milioni 10 na unavyoweza kuwajengea morali!

Najiuliza waandaaji nao, wanaridhika, kama hapana mbona ni miaka nenda rudi bado wapo walipo au wanaona panatosha? Tangu michuano hiyo ianze mwaka 2007, miaka tisa kwenda wa kumi. Vipi? Mbona kuna nafasi ya kupiga hatua na kupata wadhamini watakaofanya ikiwezekana iwe michuano mikubwa hata kupita ile ya Kagame.

Rundo la mahoteli ya Zanzibar, makampuni ya Bakhresa na mengine mengi yanayofanya biashara visiwani humo. Au yako ya Bara kwa kuwa timu za Bara zinakwenda huko ili yaongeze zawadi ikazidi mara tatu ya hapo, kukawa na zawadi ya mfungaji bora, kipa bora, kocha bora tena zawadi inayotambulika hasa.

Pia kukawa na muda mzuri wa michuano hiyo kufanyika kuepusha kusimamisha ligi ambayo inaweza kuwa athari kwa momentum (mwendo) wa timu ambazo mfano zimecheza mechi mbili za ligi mzunguko wa pili, sasa zinakwenda Mapinduzi, zikirudi inaweza ikawa tatizo kwao.


Haya ni maoni yangu, nayashikilia na ninapenda yawafikie waandaaji. Wasijifiche kwenye kivuli cha nchi, wakubali timu zinahitaji matumizi, zinawalipa mishahara wachezaji, zina gharama kubwa za uendeshaji hivyo kama wanaona zinawafaa na zinahitajika kushiriki, basi nao wanahitajika kuboresha, full stop.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic