January 9, 2017Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, ndiyo chanzo cha kipigo cha mabao 4-0 walichokipata katika mchezo dhidi ya Azam FC.

Yanga ilikutana na kipigo hicho juzi Jumamosi katika mechi ya mwisho ya makundi kwenye Kombe la Mapinduzi iliyochezwa katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kipigo hicho walichokipata Yanga, kimewaondoa kileleni kwenye msimamo wa Kundi B, wakiwa na pointi 6 huku Azam wakiongoza wakiwa na 7.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimepatikana kutoka kwa wachezaji wa timu hiyo, uchovu wa mazoezi magumu saa chache kabla ya mechi ndiyo sababu ya wao kupoteza pambano hilo.

Mtoa taarifa huyo alisema, timu hiyo siku ya mechi asubuhi walifanyishwa mazoezi kama kawaida kwa muda wa saa mbili wakati usiku wakiwa na mechi.

Aliongeza kuwa, katika mazoezi yao hayo, walifanya programu zote ikiwemo kukimbia mbio fupi (short splint), mbio ndefu na kuruka koni kabla ya kumalizia programu ya kupiga penalti, kitu ambacho siyo sahihi na badala yake walitakiwa kupumzika kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo.

“Kiukweli kabisa ilikuwa lazima tufungwe mechi na Azam, na hiyo imetokana na wachezaji wote kuwa na uchovu na kama ulifuatilia mchezo ule, utaona wachezaji wote tulikuwa tumechoka kutokana na mazoezi magumu tuliyofanya asubuhi wakati jioni tukiwa na mechi ngumu.

“Kwa mfano, mimi (jina kapuni), nilishindwa kutimiza majukumu yangu kutokana na uchovu niliokuwa nao, kwa kweli kama tukiendelea na programu hii ya siku ambayo tunacheza mechi jioni halafu tukafanya mazoezi asubuhi, basi tutaendelea kufungwa kwenye mechi hizi zijazo za Mapinduzi na ligi kuu.

"Na hiyo asubuhi yenyewe ni bora tungekuwa tunafanya mazoezi mepesi, tunafanya mazoezi magumu kwa masaa (saa) mawili kwa jana (juzi) siku ya mechi asubuhi tulikimbia mbio fupi na ndefu, kuruka koni na kumalizia na kupiga penalti kitu ambacho siyo sahihi," alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Lwandamina bila mafanikio lakini Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema: “Katika mechi hii, wachezaji waliingia uwanjani wakiwa na matumaini makubwa ya ushindi kutokana na mwenendo wa Azam katika michuano hii.

"Hivyo, dharau hizo ndizo zikatusababishia tupate matokeo hayo, lakini yote kwa yote benchi la ufundi limeangalia makosa yaliyojitokeza katika timu na kusababisha kupata matokeo hayo, hivyo tunajipanga kwa ajili ya mchezo ujao."


SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV