January 9, 2017Na Saleh Ally
YANGA wamepoteza mechi yao dhidi ya Azam FC kwa mabao 4-0. Hakuna shabiki wa Yanga aliye na furaha hata kidogo na wengi wameanza kulaumu mambo mengi sana, hakuna anayejaribu kutafakari.

Yanga wanaamini wao wana kikosi cha kushinda kila mechi, kupoteza kwao ni sare. Hili ni jambo la hovyo kabisa kuliamini kwa yeyote yule.

Niliamini Azam FC inaweza kuifunga Yanga, nilijua inaweza kuwa sare na Yanga pia inaweza kushinda. Sikutarajia Yanga inaweza kupoteza mechi hiyo kwa idadi hiyo kubwa ya mabao, lakini hakuna ajabu ndiyo soka.

Wakati mechi hiyo ikiendelea, nilikuwa nikijiuliza maswali mengi na hata baada ya mechi nilijaribu kuzirudia video kadhaa zilizorekodiwa zikiwemo zile za mabao manne, nikagundua vitu nilivyoona ni vigeni kabisa kwa wachezaji wa Yanga na kuanza kuamini bao hizo nne zilitengenezwa ndani ya Yanga huku ikiwezekana hata wao Yanga hawakuwa wakijua.

Muonekano wa uchezaji au movement appearance. Si ya kawaida, wachezaji walionekana ni wavivu, hawana kasi na walicheza kama ambao hawakuwa tayari.

Ukiangalia takwimu za mapumziko na takwimu za baada ya dakika 90, Yanga ndiyo ilikuwa chini na inakuwa mechi ya kwanza ndani ya msimu wa 2016-17 iwe ya Ligi Kuu Bara, kirafiki au Mapinduzi, Yanga kumaliza ikiwa chini kitakwimu na timu yoyote iliyocheza nayo, kwani hata ilipofungwa na Stand United na Mbeya City, bado ilikuwa bora kwa maana ya umiliki wa mpira, mashuti mengi langoni hata iliyokosa na mashambulizi mengi.

Kutomfurahia kocha:
Wakati nilipoona tofauti hiyo, niliona wazi kuna shida suala la wachezaji kutomfurahia kocha na mazoezi yake magumu kunaweza kukawa kumechangia kwa kiasi kikubwa.

Yanga inaweza ikawa imefungwa uwanjani lakini sababu zikawa zinaanzia mbali nje ya uwanja. Kwa kuwa hivi karibuni wachezaji waliwahi kulalamika kuwa wanafanyishwa mazoezi magumu lakini wakaitumia nafasi hiyo kulalamika kwamba mshahara umecheleweshwa.

Nilianza kufikiria kabla ya mechi ya Azam FC, wachezaji walifanyishwa mazoezi makali jambo ambalo liliwaudhi kwa mara nyingine.

Lakini pia, kama walifanya mazoezi makali siku moja kabla au siku ya mechi ni kosa kubwa. Miili yao isingeweza kunyumbulika na mfano mzuri angalia bao la kwanza, kipa Deogratius Munishi anapangua shuti la Joseph Mahundi, linarudi ndani na John Bocco anafunga mbele ya mabeki watatu ambao wanaonekana wamezubaa.

Angalia bao la pili, Vicent Andrew ambaye ni bora kwa vichwa lakini anashindwa kuruka vizuri na kumpa Mghana, Yahaya Mohamed nafasi ya kufunga kwa urahisi sana.

Bao la tatu, Mahundi anamuacha Dante kwa kumdanganya na mwili. Hata kabla hajapiga, muangalie Dante anavyokimbia kama mtu aliyebeba dunia mgongoni.

Bao la nne, wakati inapigwa krosi, jiulize Kelvin Yondani na Dante walikuwa wapi, lakini Geofrey Mwashiuya naye anaukosa mpira ikionyesha miili yao imekuwa migumu sababu ya fatiki kama hayo mazoezi yalikuwepo.

Angalia vizuri tena hiyo mechi, utagundua unyumbulikaji wa wachezaji wa Yanga, kasi yao pia haikuwa sawa ukilinganisha na michezo iliyopita.

Wengi walikuwa wakianguka, hawakuwa na uwezo wa kupiga pasi nyingi na hata ile sifa ya kupokonya mpira haikuwepo tena maana Azam FC wakati mwingine walipiga hadi pasi 18 na kufika langoni halafu wakashambulia.

Kipindi cha kwanza kinaisha Yanga haijapiga hata shuti moja langoni! Hakuna pasi hata moja bora ya Haruna Niyonzima au Thabani Kamusoko!

Kugomea mshahara:
Suala la wachezaji kugoma kwa kuwa walicheleweshewa mishahara, kiasi fulani linaonekana bado limewaathiri wachezaji wa Yanga. Maana mashabiki walikasirishwa nalo na kuwasakama wakiwakosoa, wao waliona mashabiki hawapo nao.

Wamejituma katika mechi kadhaa, lakini inawezekana bado ni kitu kinachowaumiza maana kilikuwa na ukweli.

Mfumo wa Yanga upo hivi; mshahara wa Januari, wachezaji wanalipwa Januari Mosi, hivyo wao wanakuwa na deni la mwezi mzima. Hivyo kweli waliona walikuwa na kosa na wameshindwa kulisahau.

Makocha wawili:
Suala la Kocha Hans van der Pluijm kuondolewa kwenye benchi, kachukua George Lwandamina na bado ndani yake kuna Juma Mwambusi aliyekuwa msaidizi wa Pluijm, hili ni kosa kama nilivyoeleza awali.

Utawala wa Lwandamina si asilimia mia, bado wachezaji wakichukizwa wana sehemu ya zamani kufikiria ilikuwa sahihi kwa kuwa ipo karibu na wanaona wanaweza kuungwa mkono.

Hili linaweza kuonekana ni la kawaida sana, lakini litaendelea kuipa Yanga wakati mgumu kila kunapotokea kosa dogo ambalo lingeweza kuonekana ni dogo kama utawala wa kocha wa sasa ungekuwa unajitegemea kwa asilimia mia.


6 COMMENTS:

 1. kwani yanga kufungwa lazima mtoe povu lote hilo, yanga ni timu kama zilivyo Jamhuri na timu zingine, mbona wanfungika tu

  ReplyDelete
 2. Huyu jamaa tathmini zake ni kigeugeu kama kinyonga. Azam waliwabana yanga ndo mana wakawafunga.. Yanga ikifungwa huwa hamkubali sijui kwanini... Mtatoa sababu nyiiingi, angalia hata issue ya mishahara umeileta hapa, mlipowafunga jamhuri na sijui nani huko mishahara na mazoezi magumu havikuwepo, leo 4G ya azam mnaweweseka. Waheshimu Azam kaka.

  ReplyDelete
 3. Huyu jamaa tathmini zake ni kigeugeu kama kinyonga. Azam waliwabana yanga ndo mana wakawafunga.. Yanga ikifungwa huwa hamkubali sijui kwanini... Mtatoa sababu nyiiingi, angalia hata issue ya mishahara umeileta hapa, mlipowafunga jamhuri na sijui nani huko mishahara na mazoezi magumu havikuwepo, leo 4G ya azam mnaweweseka. Waheshimu Azam kaka.

  ReplyDelete
 4. Mi nafikiri ni mtazamo tu ila mpira una falsafa yake huwezi sema mazoez magumu wakat ukiwa uwanjani unaokana dk tisini haupo fiti sema wachezaji wakibongo hawajielewi na kujua mpira ni ajira tosha usipojishughulisha utashughulishwa .Tuache kupeana moyo maendeleo huja kwa mipango.

  ReplyDelete
 5. "kwani hata ilipofungwa na Stand United na Mbeya City, bado ilikuwa bora kwa maana ya umiliki wa mpira, mashuti mengi langoni hata iliyokosa na mashambulizi mengi"
  Hapa umesahau ilipocheza na Azam takwimu zilikuwa Azam 52% Yanga 48%. Hata 01 Oct na Simba walizidiwa Takwimu.

  ReplyDelete
 6. Muandishi anaipenda sana Yanga, anajaribu kuelezea kuwa ni Timu nzuri na haikustahili kufungwa.

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV