February 24, 2017Mlinda mlango wa Kagera Sugar, Juma Kaseja, amewapiga kijembe wote wanaosema kuwa umri umemtupa mkono kwa kuwaambia waendelee kuzungumza wakati yeye anakusanya tuzo tu.

Kaseja ametoa kauli hiyo baada ya juzi Jumatano kutangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa ndiye mchezaji bora wa Januari kutokana na mchango wake mkubwa aliouonyesha katika timu yake kwa mwezi huo.

Akiizungumzia tuzo hiyo, Kaseja amesema: “Kwanza kabisa namshukuru sana Mungu, naishukuru familia yangu, Benchi la Ufundi la Kagera Sugar, viongozi, wachezaji wenzangu na mashabiki wote wa Kagera Sugar kwani ushirikiano na umoja wetu ndiyo umeifanya hiyo tuzo leo hii ije Kagera.

“Watu wamekuwa wakisema Kaseja umri umekwenda, lakini nadhani wanaochagua mchezaji bora wa mwezi wanaangalia vigezo na vigezo hivyo huwa vinapatikana uwanjani, kwa hiyo mimi sina mengi ya kuongea bali nitaendelea kuonyesha vitu vyangu uwanjani na kiwango changu ndicho kitaifanya tuzo hiyo irudi tena Kagera.

“Najua ni watu wachache ambao wameamua kuongea uongo na kuwaaminisha wengi kwamba sina uwezo, binafsi siwezi kuwazuia kuongea, wanatakiwa kufahamu kwamba mimi ni mchezaji na ili mchezaji aonekane mzuri basi anaangaliwa uwanjani anafanya nini kwa sababu soka linachezwa hadharani na si chumbani.”

Katika hatua nyingine, Kaseja amesema kuwa, siri ya yeye kuendelea kuwa bora ni kumuomba Mungu, kufanya mazoezi na kufuata kile anachofundishwa na makocha wake na kukifanyia kazi.

SOURCE: CHAMPIONI


1 COMMENTS:

  1. Afanye kazi yake asibishane na mashabiki au viongoz flan, mpira na kuongea ni vtu tofaut kiwango kina mwsho lkn kuongea watu wanaongea tu lbd mtu afe

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV