February 11, 2017




Na Saleh Ally
MARA ya mwisho vigogo Liverpool kubebwa ubingwa wa Ligi Kuu England ni msimu wa 1989-90, ikijulikana kama Ligi Daraja la Kwanza.


Kuanzia hapo hadi sasa miaka ya 2000, utamu wa ubingwa kama ni harufu, inatokea kwa majirani. Liverpool ndiye kigogo aliyekaukiwa taji hilo muda mrefu zaidi kuliko mwingine.


Nahodha wake maarufu, Steven Gerrard, amezaliwa, akakulia hadi kukomaa kisoka ndani ya Liverpool lakini hadi anaondoka kwenda Marekani, hakuligusa kombe hilo.


Msimu wa 2013-14 ilionekana kama wanalichukua, mwisho wakaishia kuteleza mwishoni na Man City akafikisha pointi 86 na kuwa bingwa. Msimu uliofuata bingwa akawa Chelsea na pointi 87 (Liverpool ikawa ya saba), Msimu uliopita bingwa Leicester na pointi 81 (Liverpool ikamaliza ya 8).


Kocha Jurgen Klopp alimaliza msimu uliopita nafasi ya 8, alivyoanza msimu huu ikaonekana hakuna wa kumzuia lakini sasa ligi inakwenda ukingoni, yuko nafasi ya 5 na hofu ya kuteremka zaidi imezidi. Yaani Liverpool imepoteza nguvu ya kuvuta kwenda juu au pull kama wasemavyo Waingereza.


Ukiangalia nimekutengenezea msimamo hadi mapumziko. Liverpool inashika nafasi ya pili baada ya Chelsea.


Yaani ilikuwa inaongoza kwa mabao hadi mapumziko. Hivyo kila mechi, imepewa pointi tatu kwa maana ya ushindi wa dakika 45 za kwanza.


Katika mechi 24 walizocheza hadi mapumziko, 12 walishinda, 7 wakatoa sare na 5 walipoteza ikiwa na maana pamoja imekuwa ikiporomoka kitakwimu.



Katika mechi 24 za ligi, Liverpool imeshinda 19. Kati ya hizo, 12 walishinda baada ya kuongoza hadi mapumziko lakini tano walishindwa na 7 mwisho wakaenda kupata sare.


Mwendo wa Liverpool umeendelea kuporomoka kila kunapokucha. Wanapoteza ‘touch’ ya aina ya uchezaji wao, aina yao na sasa wanaanza kuhaha.


Nachukua mechi 13 walizoshinda, 7 wameshinda nyumbani na 6 ugenini. Huu ni uwiano mzuri na utaona wamepata sare tatu nyumbani na 4 ugenini, huu ni uwiano bora mwingine kama walivyopoteza 3 ugenini na moja nyumbani.


Sasa unajiuliza, wapi wanapopoteza aina yao iliyowafanya kuwa vinara wa ligi na sasa wameporomoka hadi nafasi ya tano?


Sifa ya Liverpool ilikuwa ni mabao mengi ya ushindi. Baada ya kuifunga Stoke City 4-1, hiyo ilikuwa Desemba 27, mwaka jana, halafu wakafunga mwaka Desemba 31 kwa kuitwanga Man City 1-0. Mwaka huu umeonekana si wao na mambo hayaendi katika mwendo wanaoutaka au walioupangilia.


Januari 2, walikuwa ugenini dhidi ya Sunderland. Matokeo yakawa sare ya 2-2, kumbuka hii ndiyo ilikuwa mechi yao ya kwanza ya mwaka 2017.


Mechi iliyofuata Januari 15, wakawa ugenini tena Old Trafford dhidi ya Man United, wakaambulia sare ya bao 1-1 na ndani ya mechi mbili za 2017, wakawa wamedondosha pointi nne.


Januari 21 wakarejea nyumbani Anfield, wakakutana na kipigo kutoka kwa Swansea cha mabao 3-2. Ikawa wameangusha jumla ya pointi 7 ndani ya mechi tatu.


Januari 31, wakabaki Anfield kuwakaribisha vinara wa Premier League, Chelsea. Mwisho ikawa 1-1 wakiangusha pointi nyingine mbili na kuwa tisa kwa Januari pekee.



Februari 4, wakakutana na Leicester City na kuchapwa 2-0 wakiwa ugenini. Kwa mwaka huu tu wameangusha jumla ya pointi 11 kutokana na sare au kufungwa huku wakiwa hawajashinda hata mechi moja ya Premier League.



Inaonekana Liverpool iliyomaliza mwaka 2016 si hii ya 2017! Au Klopp anakosea wapi na kipi alikifanya mwaka uliopita na anashindwa kukifanya mwaka huu?



Sadio Mane kwenda kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kuitumikia Senegal na Coutinho kutokuwa vizuri ndiyo sababu? Wako wengi kama Firmino au Adam Lallana ambao wanaweza kufanya makubwa.


Kinachoonekana ni Liverpool kupoteza mwelekeo hasa mwishoni. Waingereza wanasema “Out of same touch”. Kwamba Liverpool kushindwa kushikilia mwendo wake wa kufunga mabao mengi katika kila mechi.


Hii ndiyo ilikuwa sifa namba moja, ukitaka kuhakikisha hilo, angalia msimamo; Liverpool iko katika nafasi ya tano lakini ndiyo timu inayoongoza kwa mabao ya kufunga, ina 52 sawa na Arsenal, inafuatiwa na vinara Chelsea wenye 51.


Hadi Arsenal kuifikia au Chelsea kuikaribia ni kutokana na kusuasua baada ya kuanza mwaka 2017. Ilifikia ikiwa katika nafasi ya pili, ilikuwa na mabao ya kufunga 10 zaidi ya Chelsea.


Mwendo huu ni sahihi kwamba Liverpool inaporomoka na kama itasonga na mwendo huu ndani ya mechi tatu tu zijazo, ishu ya ubingwa itakuwa si yake tena, labda kwa miujiza.


Unaweza kusema wana bahati mbaya kwa kuwa wanakutana na Tottenham ambao wako vizuri. Wakishinda wataangusha mabawa manne ya ndege wawili kwa kuwa Spurs ni mpinzani wao ndani ya Top Four.


Kujikomboa kwa Liverpool ni lazima kushinda mechi mbili ndani ya tatu zijazo na kama ikiwezekana basi kushinda zote tatu.

Kingine kikubwa anachotakiwa kufanya Klopp ni kubadili aina ya mwendo. Inaonekana kama amekuwa hana plan B au mpango mbadala kwa kuwa wamemsoma na wanaelewa anafanya nini hasa baada ya kuwanyanyasa katika mzunguko wa kwanza.

Uchaguzi unabaki kwa Liverpool. Mashabiki wanaonekana tayari wamekata tamaa. Kwa wachezaji au kocha kukata tamaa haiwezi kuwa hadithi sahihi hata kidogo.

Lazima Klopp aliingize jeshi lake katika Plan B, au akubali kugombea kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

MSIMAMO WA HADI MAPUMZIKO
                                      GP       W     D      L       Pts
1. Chelsea                     24        15    5       4       50
2. Liverpool                 24        12    7       5       43
3. Man City                  24        12    6       6       42
4. Arsenal                     24        10    11    3       41
5. Man Utd                   24        10    9       5       39
6. Tottenham                24        9       10    5       37
7. West Brom               24        7       12    5       33
8. Stoke City                24        8       8       8       32
9. Bournemouth           24        8       8       8       32
10.  West Ham            24        7       11    6       32


TAKWIMU 2016-17
Chelsea wamecheza mechi 9 bila kupoteza hata moja
Tottenham hawajapoteza mchezo katika mechi zao 9 zilizopita
Manchester City wamefunga kwa 100% mechi za nyumbani
Arsenal wamefunga bao kwa 92% mechi za ugenini
Liverpool wamefunga mabao kwa 91% mechi za nyumbani


TAKWIMU 2015-16
Leicester City hawakupoteza mechi 12 za mwisho wakawa mabingwa
Arsenal hawakupoteza katika mechi 10 za mwisho
Tottenham walifunga mabao 89% mechi za ugenini


TAKWIMU 2014-15
Chelsea haikufungwa mechi zake 19 za mwisho za ligi, ikabeba ubingwa
Manchester City walishinda mechi zao 6 za mwisho
Arsenal walishinda mechi zao 6 za mwisho


TAKWIMU 2013-14
Manchester City ilibeba ubingwa baada ya kushinda mechi 5 za mwisho
Liverpool haikupoteza katika mechi zake 9 za mwisho ugenini
Chelsea ilishinda mechi zao 3 za mwisho, haikubeba ubingwa

Arsenal ilishinda mechi zake 5 za mwisho, haikuwa bingwa pia

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic