February 6, 2017



Matarajio ya beki wa kati wa Simba Mganda, Juuko Murshid kurejea kwenye timu hiyo yamepotea baada ya kupata dili la kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya Red Star Belgrade ya nchini Serbia.

Beki huyo, hivi sasa yupo nchini Uganda baada ya kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Uganda ilipokwenda Gabon kucheza Afcon.

Mganda huyo aliondoka kwenye timu hiyo na kurejea Uganda, tangu kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha Uganda kinachonolewa na Mserbia, Milutin Sredojević 'Micho’.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, beki huyo wakati wowote atajiunga na klabu hiyo ambayo iliwahi kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mtoa taarifa huyo alisema, uongozi wa Simba umemruhusu beki huyo kujiunga na klabu hiyo kwa lengo ya kujipatia fedha kutokana na mkataba aliobakiza kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Aliongeza kuwa, meneja wa beki huyo hivi sasa yupo kwenye mazungumzo ya mwishoni kwa ajili ya kujiunga na Belgrade waliowahi kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la Europa na Super Cup.
"Juuko hatarejea tena kuichezea Simba kwenye mechi hizi zilizobaki za ligi kuu kama inavyoelezwa, hiyo ni baada ya ofa nzuri ya Klabu ya Belgrade ya Serbia.
"Uongozi wa Simba umetoa baraka zote za beki huyo kuondoka ili wapate fedha za usajili, kwani mchezaji huyo anapouzwa, Simba itafaidika kwa mauzo ya mchezaji, kwa kuwa bado ana mkataba na Simba.
“Simba wamemruhusu kuondoka kutokana na muda mchache alioubakiza kwenye mkataba wake ambao unafikia kikomo mwishoni mwa msimu, hivyo kama Simba wakimuachia mwishoni mwa msimu hawatafaidika chochote, hivyo wameona wamruhusu kipindi hiki ili wapate fedha," alisema mtoa taarifa huyo.
Hata hivyo, alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe, alisema hawana mpango wa kumuachia aondoke na badala yake ataendelea kuwepo kikosini hapo.

Juuko tangu alipoondoka Simba Novemba, mwaka jana, hajarejea nchini kujiunga na wenzake.

“Juuko bado ni mchezaji wetu na ataendelea kuwa wetu mpaka pale mkataba wake utakapomalizika. Kutorejea kwake haraka hilo hata lisiwashtue watu, muda wowote anaweza kurudi na kuungana na wenzake,” alisema Hans Poppe.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic