February 25, 2017Hii leo Jumamosi Simba na Yanga zinashuka uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lakini suala la tiketi limezua mambo.


Ni kwamba, mashabiki wa timu hizo mbili wameonekana kugomea baada ya mauzo ya tiketi mpaka kufikia jana jioni kusuasua tofauti na ilivyotarajiwa.


Meneja Miradi wa Kampuni Selcom inayosimamia zoezi la uuzaji wa tiketi za mechi hiyo, Gallus Runyeta amesema kuwa, mpaka kufikia muda huo walikuwa wameuza tiketi zisizozidi 30,000 ukilinganisha na idadi ya kadi za kununulia tiketi hizo walizozitoa kwa mashabiki hao.


“Mambo siyo mazuri kabisa kwani zoezi la tiketi linasua kabisa na ukizingatia mechi inachezwa kesho (leo), kwani mpaka sasa tumeshauza tiketi zisizozidi 30,000 tu.


“Tangu utaratibu wa kuingia uwanjani kwa mfumo huu wa tiketi za kielektroniki tumeshatoa kwa mashabiki kadi za kununulia tiketi za kuingilia uwanjani zaidi ya 200,000,” alisema Runyeta na kuongeza kuwa:


“Tiketi tunazotakiwa kuuza kwa mashabiki ni 57,310 lakini hadi sasa tumeuza idadi hiyo ya tiketi, sijui tatizo ni nini. Tumeshawasiliana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwataarifu juu ya hilo,” alisema Runyeta.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV