Huku kikosi cha Yanga kikishuka dimbani leo kuivaa Simba, Mwenyekiti wake, Yusuf Manji jana alikuwa akihojiwa na Jeshi la Uhamiaji kuhusu tuhuma za kuwa na hati za kusafiria za nchi mbili.
Habari zinasema kwamba, Manji jana alitumia karibu kutwa nzima katika ofisi za Uhamiaji akihojiwa na hakukuwa na taarifa yoyote ile kuhusu kufikishwa mahakamani au vinginevyo. Hadi saa 9:00 alasiri chanzo chetu kilidai Manji alikuwa bado anahojiwa. Hii ni mara ya pili anahojiwa ndani ya wiki moja.
Mmoja wa watu wa karibu wa Manji amesema kuwa, Manji jana alianza kuhojiwa na Uhamiaji asubuhi halafu kukawepo na taarifa taarifa za kufikishwa mahakamani lakini Uhamiaji haikutoa taarifa yoyote kuhusu suala hilo hadi jana usiku.
“Manji amepelekwa Uhamiaji kwa mahojiano labda akitoka huko ndipo anaweza kwenda mahakamani, lakini Uhamiaji hawajatueleza jambo lolote lile,” alisema.
Baada ya gazeti hili kusubiri kwa muda mrefu kujua hatima ya Manji, tulipokitafuta tena chanzo chetu kilisema;
“Bado anahojiwa na Uhamiaji na hatujui nini kitatokea lakini leo na ataendelea kuwa chini ya ulinzi kwani atarudi tena hospitalini.”
Hii ina maana Manji atabaki Hospitali ya Aga Khan chini ya uangalizi wa Uhamiaji hivyo leo hatokuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishuhudia Yanga ikicheza dhidi ya Simba katika Ligi Kuu Bara.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment