February 10, 2017
Siku 15 kabla ya mchezo wa Simba dhidi ya Yanga katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, huku Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikidai kuwa mwamuzi wa mchezo huo atakuwa chipukizi, gazeti hili limepata uhakika juu ya mwamuzi huyo.


Timu hizo zitapambana Februari 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, tayari presha imeshaanza kuwa kubwa juu ya mwamuzi atakayechezesha mchezo huo hasa baada ya TFF kutangaza kuwa atakuwa chipukizi ambaye hajawahi kuchezesha mchezo baina ya timu hizo. 


Habari za uhakika ambazo gazeti hili imezipata kuwa mwamuzi huyo ni Elly Sasi wa Dar es Salaam ambaye inaaminika kuwa uwezo wake wa kuchezesha umekuwa ukiboreka kiasi kwamba ameaminiwa na kupewa mchezo huo.

Mwamuzi huyo chipukizi ndiye ambaye alichezesha mchezo wa Simba dhidi ya Azam katika raundi ya kwanza ya ligi hiyo msimu huu.

“Kijana ni mzuri, anaweza kuchezesha, anajiamini na anafanya maamuzi bila hofu, nadhani watamtangaza yeye labda kama nyie mkitoa habari hii kisha wao wakaamua kubadili maamuzi yao,” kilisema chanzo na kuongeza:

“Tatizo la hawa waamuzi chipukizi akiwemo yeye ni kuwa kuna wakati wanajiona wameshamaliza kazi, wanataka kujiona bora na kutosikiliza wakubwa zao lakini kiuwezo kijana yuko vizuri.”

Chanzo hicho kilipoulizwa sababu za TFF kutowapa mchezo huo waamuzi wakongwe kilisema: “Sijui sababu lakini mtu kama (Israel) Nkongo anataka kustaafu mwakani, aliukataa mchezo huo.”

Kwa miaka ya hivi karibuni, mechi za Simba na Yanga zimekuwa na kawaida ya kuchezeshwa na waamuzi wakongwe kama Martin Saanya na Nkongo pamoja na Jonensia Rukyaa.

Mapema wiki hii, Mwenyekiti wa Frat, Nassor Mwalimu alinukuliwa akisema:

“Mwamuzi tunayemtarajia kumpanga ni chipukizi kabisa ambaye ndiyo kwanza amechezesha katika mzunguko wa pili kuna waamuzi kama wanne hivi tulikuwa tumepeana majukumu ya kuwafuatilia kwa kina.”

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV