February 6, 2017



Na Saleh Ally
SUALA la haki wakati mwingine unaweza kulichelewesha tu lakini mwisho ukweli huwa unapatikana na mwenye haki yake anaipata, wala hakuna mjadala.


Congo Brazzaville walitaka kuidhulumu Tanzania katika michuano ya vijana chini ya miaka 17 kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika. Lakini mwisho imeshindikana.


Congo wanajua walimchezesha Langa Lesse Bercy ambaye alikuwa ni kijeba. Baada ya ushindi wa 3-2 jijini Dar es Salaam, Congo nao wakashinda kwa bao 1-0 tena katika dakika za mwisho kabisa mfungaji akiwa huyo kijeba.


Juhudi za kutaka kupatikana kwa vipimo vya vinasaba yaani DNA zilifanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kufuata taratibu za lile la Afrika (Caf) na mwisho Congo walishindwa kutimiza masharti na Serengeti ikatangazwa kufuzu.


Nianze kutoa pongezi zangu kwa TFF kwa mambo mawili, hata kama walikuwa wakiwahudumia vijana hao kwa fedha za msaada kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), lakini wamejitahidi kufanya vizuri na vijana wamefuzu.


Pili niwapongeze vijana wenyewe ambaowamefanya kazi nzuri sana. Hawa wanakuwa mfano wa vijana bora wanaojitambua, ninawaomba wawe na nidhamu waendelee hivi na zaidi kwa maana ya kupambana wakitaka mafanikio, hakuna shaka mafanikio makubwa yanakuja mbele yao.


Tatu ni benchi la ufundi, nianze na Bakari Shime, Mtanzania aliyepewa jina la Mchawi Mweusi. Hakika amefanya kazi kubwa na anastahili sifa kuu. Deni kubwa kwake ni michuano iliyo mbele yake.


Mwisho pongezi hizi ningependa Rais wa TFF, Jamal Malinzi anifikishie hizi salamu, kwa mtu ambaye mimi namuona ndiye “mchawi” hasa na tumekuwa tukimsahau hata kumpa pongezi timu inapofanya vizuri.

Kocha Kim Poulsen, huyu ndiye bosi wa benchi la ufundi la kikosi cha Serengeti Boys. Hakika kazi yake ni bora na ana uwezo mkubwa sana.


Kwa mnaokumbuka, aliletwa wakati TFF ikiwa chini ya uongozi wa Leodeger Tenga na baada ya hapo kulikuwa na mabadiliko makubwa, mfano mzuri ni Simon Msuva na Frank Domayo waliopitia mikononi mwake. Lakini kwa kundi kubwa la vijana ambao sasa ni tegemeo kwenye timu zao na timu ya taifa.


Kama mnakumbuka, baada ya uongozi wa Malinzi kuingia madarakani ulianza kuondoa kila kilichoonekana ni cha Tenga. Poulsen wakati huo alikuwa kocha wa Taifa Stars. Akaondolewa na kuletwa Mart Nooij ambaye aliboronga ile mbaya.


Hakukuwa na sababu ya kumuondoa Poulsen na ukumbuke TFF ililazimika kumwaga takribani Sh milioni 50 kumlipa na kuvunja mkataba. Akaondoka na mambo yalipokuwa magumu, huenda kwa mara ya kwanza, Malinzi akaona alipokosea na kumrejesha.


Pamoja na kwamba TFF ilikula hasara zile fedha ilizomlipa kuvunja mkataba, huenda ingezitumia kufanya mambo mengi ya maana kama kungekuwa na ufikiri wa busara  basi kocha huyo angepewa timu ya vijana badala ya kumuondoa kwa kuwa tu aliletwa na Tenga.

Lazima tukubali kwamba Poulsen ni kati ya makocha bora na wanaoijua vizuri kazi ya kuwanoa vijana. Kazi yake ni bora na ndiye msaada mkubwa kufikia hapo ilipo.


Inawezekana wengi wanachukulia kufuzu Afcon ya vijana ni kama jambo la kawaida, lakini naamini hii ni njia sahihi zaidi kuliko ingefuzu timu kubwa kwa kuwa itakaposhiriki michuano hiyo, tutaanza kujenga msingi taratibu.


Vijana hao wakishiriki michuano hiyo wataimarika zaidi, watajitangaza na huenda watapata timu kama watafanya vizuri zaidi na baada ya miaka kadhaa watakuwa ni watu wenye hamu ya kushiriki michuano ya Afcon ya wakubwa.



Tena watakuwa na nafasi ya kuisaidia Tanzania kufuzu kwa kuwa watakuwa wanatokea katika timu kubwa au za Ulaya ambazo zitakuwa zimewapa mafunzo bora. Hivyo Malinzi, nimekupongeza lakini nifikishie hizi pongezi kwa Poulsen.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic