February 15, 2017Na Saleh Ally
BAADA ya timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, kinachoanza sasa ni maandalizi.


Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kambi itakuwa nje ya nchi kwa ajili ya kuhakikisha inakuwa katika maandalizi bora.


Tunakumbuka timu hiyo iliwahi kuweka kambi nje ya Tanzania, ilikuwa nchini Madagascar na vijana wakajiandaa na kufanikiwa kufuzu.


Wako ambao wamekuwa wakiamini Serengeto Boys kama imesaidiwa, lakini ukweli ni kwamba Congo waliweka dhuluma lakini mwisho haki imepatikana na vijana wamefuzu na kuingia kwenye hatua waliyostahili.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amekuwa waziri wa kwanza anayehusiana na michezo kuwa active, yaani anayeza kuendana na kasi ya michezo.Michezo ina kasi kubwa katika kila Nyanja. Unaweza kuona ajabu, lakini ukweli yule anayehusika na michezo anatakiwa kuwa mwepesi na mwenye maamuzi ya haraka. Mara nyingi wanaofanya shughuli za michezo wamekuwa wepesi katika utekelezaji.


Mawaziri wengi walishindwa kwenda na kasi ya michezo, tofauti na Nape ambaye ameonyesha mfano mkubwa na unaweza kusema hatua zake zimekuwa ni za harakaharaka sana na mambo mengi ameyafanya kwa muda mfupi.


Leo nimeandika kueleza namna ambavyo nimeona Nape akishiriki katika michezo na hasa kuhusiana na kusaidia mambo kadhaa bila ya kujitokeza.

Mfano nini kifanyike kwa vijana hao, kuwaomba watu wajitokeze kuwasaidia na kadhalika. Jambo ambalo ninaipongeza serikali kupitia Nape kwamba wameonyesha kuwajali vijana ambao nao wamewalipa.


Lakini naona huu ndiyo wakati mzuri wa serikali kusimama tena si ikibaki chini na kusukuma. Badala yake itangulie mbele na ikiwezekana suala la Serengeti Boys liwe la kitaifa na kwa pamoja tuisaidia hii timu ya vijana.Kama unakumbuka, juzi niliwashauri TFF kuweka hadharani kwamba wana kiasi gani, kiwe cha msaada au walichokusanya na baada ya hapo watueleze wadau wamepungukiwa kiasi gani badala ya kusimama hadharani na kusema Sh bilioni moja pekee ndiyo inatakiwa.


Nilitaka vitu vingi viwe vya uwazi huku nikikumbusha kuondoa suala la hofu. Kwa kuwa kuna fedha nyingi za wadhamini au wafhadhili na kumekuwa na hali ya hofu baada ya kuwa tumeelezwa mahesabu yana walakini na kadhalika.


Katika hili la kuichangia Serengeti Boys lazima kuwe na umakini yakinifu kwa kuwa kama serikali itawaacha TFF peke yao na hapa tunazungumzia michango, basi huenda hofu ikachangia wengi wasichange.


Kama hakutakuwa na michango ya kutosha kutokana na hofu, basi wengi tutaiangusha Serengeti Boys ambayo ni timu mali yetu na wala si ya TFF.


Ndiyo maana nimeamua kuweka msisitizo na kuiomba  serikali isimame imara tena msitari wa mbele na ikiwezekana Nape awe kama mwenyewe ili wadau waingie msituni kusaka mchango na kuwashawishi wadau kuichangia timu yetu.


Suala la serikali kuipigania Serengeti Boys haliwezi kuwa geni. Kweli imefanya lakini mimi naona bado haitoshi na juhudi kuu zinahitajika kuhakikisha vijana wanakwenda wakiwa na ari ya juu zaidi na ikiwezekana walionuia kufanya vizuri.


Wanapokwenda ni pagumu kuliko walipotoka kwa kuwa bora ndiyo wanakwenda kukutana huko. Hivyo watakutana na walio bora kuliko waliowafunga au kuwavuka. Hii haitakuwa kazi rahisi kwa vijana hawa.


Tukubali wanahitaji msaada mkubwa kuliko wa awali, wanahitaji kuhudumiwa na kuandaliwa kwa kiwango cha juu ilivyokuwa awali. Na serikali ikiamua, kamwe haitashindwa kutekeleza hilo na vijana wetu wakaenda Afcon wakiwa na ari ya juu.


Hawa vijana ndiyo nguzo au gia ya mabadiliko ya mchezo wa soka nchini. Hawa ndiyo mashujaa wetu wa baadaye na watatuondoa hapa topeni tulipokwama.


Hivyo namshauri Nape asimame mbele kama kamanda au dereva, tuwapiganie vijana na wadogo zetu tukiamini wakihamasika, watafanya vizuri kwa kuwa tayari wametuonyesha ni watu wenye kunuia na wanatekeleza lakini watakuwa mabadiliko ya mchezo huo hapa nyumbani hapo baadaye.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV