March 1, 2017
Beki wa Yanga,Vincent Bossou amefungukia juu ya madai yake ya mshahara ambayo anaidai klabu yake hiyo unaokadiriwa kufikia miezi mitatu sasa kwani hajalipwa tangu Desemba, mwaka jana.


Kutokana na kutolipwa huko, beki huyo aligomea kucheza mechi dhidi ya Simba akiwa anaendelea kuushinikiza uongozi wa timu hiyo umlipe stahiki zake hizo.

Bossou raia wa Togo amesema kwamba amekuwa akishangazwa na jinsi watu wanavyopotosha ukweli wa malipo yake wakisema ameshindwa kuwa mvumilivu kama wachezaji wengine jambo ambalo siyo kweli kutokana na wenzake wote kulipwa mishahara yao huku yeye pekee akiwa hajalipwa.


“Watu wanapotosha juu ya kulipwa kwangu, mimi sijalipwa kwa muda wa miezi mitatu sasa na hakuna ambaye anajali kuhusiana na mimi licha ya kwamba awali nilijitoa kwa moyo kucheza na kuipambania timu yangu.


“Malipo yangu inaonyesha tayari yameshalipwa lakini kuna baadhi ya viongozi hapo kati wanajua fedha zangu zilipo aidha zimeliwa au vipi.

 Kila siku napigwa danadana wakiniambia nitalipwa lakini mpaka sasa imefika mwezi wa tatu hakuna kitu chochote kilichofanyika.


“Ishu hii ilianzia tangu mechi na Ndanda (Desemba 28, mwaka jana), niliomba nilipwe kwa sababu naenda Gabon kushiriki Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), lakini halikufanyika jambo hilo, niliporudi nikacheza mechi zilizofuata hadi ile ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Ngaya, wakaniambia baada ya mechi nitalipwa lakini hilo nalo halikufanyika.


“Baada ya hapo nikaona hakuna sababu ya kucheza wakati sijalipwa mishahara yangu ya miezi mitatu ambayo sehemu kubwa naitumia kutoa msaada kwa watoto yatima nyumbani Togo, ndiyo nikawaambia kwamba sitacheza mechi zinazokuja hadi nilipwe fedha ninazodai lakini mazoezi nimekuwa nikifanya na wenzangu, ieleweke hivyo na hakuna jambo lingine lolote zaidi ya hilo.


“Nikiwapigia simu viongozi wanakata na hata meseji hawanijibu sasa katika hali ya kibinadamu mimi nachukizwa na hilo bora waseme ukweli kwamba fedha zangu ziko wapi,” alisema Bossou.      

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV