March 17, 2017Na Mwandishi Wetu
WAKATI Ligi Kuu Bara ikiwa inakwenda ukingoni, Simba ipo kileleni kwa tofauti ya pointi mbili tu dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga.

Pamoja na kwamba ni tofauti ya pointi mbili pekee, Simba wanajiamini wana nafasi kubwa ya kubeba ubingwa katika mechi sita zilizobaki.

Kwa sasa hesabu ya Simba ni zile mechi za Kanda ya Ziwa ambako itasafiri kwenda Kagera kuivaa Kagera Sugar, baadaye itarejea jijini Mwanza kuzivaa Mbao FC na Toto Africans.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, anaamini ligi ni ngumu sana lakini hakuna cha kuizuia Simba kubeba ubingwa.

Hans Poppe anaamini lazima mechi zilizobaki zitakuwa na figisu kutoka kwa karibu kila timu inayotaka kubeba ubingwa au kuokoka kuteremka daraja, lakini Simba itakachofanya ni kubeba ubingwa.

Hans Poppe alipoulizwa kipi kinamfanya aamini wao wanaweza kubeba ubingwa wakati waliwahi kuwa na tofauti ya pointi nane, sasa zimebaki mbili pekee, alisema.
“Tungeweza kubaki na pointi nane au zaidi, lakini kuna wachezaji walituvuruga na kusababisha tupoteze pointi nyingi muhimu,” anasema Hans Poppe.SALEHJEMBE: Waliwavuruga vipi?
Hans Poppe: Mpira wa Tanzania una mambo mengi sana, yalipita hayo na sasa tunaangalia mbele. Ndiyo maana unaona kuna ambao tuliachana nao?

SALEHJEMBE:Kikosi chenu kinaendelea na ziara za mikoani, faida yake nini kwenu?
Hans Poppe: Ligi sasa imesimama, lakini timu lazima iendelee kuwa pamoja na unajua tuna mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Madini FC. Lazima tuendelee na maandalizi.

SALEHJEMBE:Maandalizi mikoani, tena na timu nyingine za vijiji?
Hans Poppe: Nafikiri hamjaelewa, sisi hatufanyi mazoezi kwa ajili ya ushindi. Ni kama burudani lakini tunaendelea kuiweka timu yetu pamoja.

SALEHJEMBE:Kusimama kwa ligi takribani mwezi, hauoni kunachangia kuwarudisha nyuma kwa maana ya kasi?
Hans Poppe: Kabisa, ndivyo ilivyo kwa kuwa ligi imesimama wakati mambo yamechanganya. Ila sisi tumekuwa na busara, badala ya kuanza kulaumiana, tumeamua kuendelea na mazoezi na ndiyo maana tunaendelea na ziara yetu.SALEHJEMBE: Lini mwisho wa ziara hiyo?
Hans Poppe: Itaendelea tu hadi tutapofika Kagera. Tunaweza kwenda Mara na kwingineko. Hapa tunatafuta kuwa fiti na kumaliza kileleni mwa ligi.

SALEHJEMBE:Nakumbuka uliwahi kulalamika kwamba Laudit Mavugo anacheza kizembe, wewe ndiye ulimsajili. Sasa unamuonaje?
Hans Poppe: Kweli nilisema na kila mmoja alikuwa akiona mwenendo wake. Sasa ni Mavugo hasa ambaye tulikuwa tunamtarajia.

SALEHJEMBE: Nini hasa kimembadilisha?
Hans Poppe: Simba ina mbinu nyingi, tulishirikiana na kumuweka chini, kuzungumza naye na mwisho umeona naye ameongeza juhudi. Mfano siku ya Yanga, alinifurahisha sana sehemu moja.

Championi: Sehemu ipi hiyo?
Hans Poppe: Pale aliposepa na kijiji (kicheko).

SALEHJEMBE: Alisepa na kijiji? Vipi?
Hans Poppe: Alichukua mpira katikati ya wachezaji wanne wa Yanga, akaondoka nao karibu na katikati ya uwanja. Halafu akaachia shuti kali sana, bahati yake sana huyo Dida.

SALEHJEMBE: Wakati Mavugo anaanza kuonyesha cheche zake. Shiza Kichuya naye amerejea na kuwa msaada tena. Mmefanya nini kuhakikisha anarejea?
Hans Poppe: Simba ndiyo sehemu viongozi wanaweza kujua haraka nini cha kufanya kutokana na mazingira ya mchezaji.

SALEHJEMBE: Kwa Kichuya mliangalia kipi, mlifanya nini?
Hans Poppe: Unajua kilichomponza Kichuya?

SALEHJEMBE: Hapana, nieleze tafadhali.
Hans Poppe: Wakati anatokea Mtibwa Sugar, sisi hatukusajili mfungaji. Tulitaka mtengeneza mabao kama ambavyo alikuwa akifanya huko. Sasa baada ya kuja Simba, akaanza kufunga. Mwisho akajisahau na kuona ni kazi yake. Aliposhindwa kufunga, naona ikamuathiri kisaikolojia.

SALEHJEMBE: Kwa hiyo kabadilika kwa kuwa sasa hatakiwi kufunga?
Hans Poppe: Hapana, anaweza kufunga akipata nafasi lakini kazi yake kubwa ni kuhakikisha anatengeneza. Pia ameelezwa kucheza mpira wake anaoujua. Nafikiri ulimuona siku na Yanga.

SALEHJEMBE:Alifanyaje?
Hans Poppe: Alipoingia yeye ndiye alikuwa anaharibu ‘move’ za Yanga kwa wingi sana. Kama haitoshi alichukua mipira na kusukuma mbele na utaona alikuwa anacheza mpira wake hasa.

SALEHJEMBE:Umemuona kijana wenu wa zamani, Hassan Kessy sasa anaonyesha uwezo mkubwa?
Hans Poppe: Acha aonyeshe, sisi haituhusu ila watupe mpunga (fedha) wetu.


SALEHJEMBE:Lakini TFF imeishapitisha mlipwe Sh milioni 50, lazima mtalipwa, hofu yenu nini?
Hans Poppe: Ishu yetu ilipitishwa kabla tulipwe Sh milioni 50, TFF haijawahi kuzikata fedha za Yanga kutulipa na inazo lakini wengine inakata za kwetu inawalipa.

SALEHJEMBE: Mmekatwa wapi, nani kalipwa?
Hans Poppe: Kuna kocha alisema ana mkataba na Simba, sisi mkataba hatuutambui, hukumu imepitishwa sisi hatupo kikaoni, wakasema alipwe Sh milioni 17 na tayari fedha zetu zimeishachukuliwa, hii ni ajabu kabisa!

SALEHJEMBE:Kumbuka sheria ni msumeno.
Hans Poppe: Basi ikate kotekote. Maana naona kama kuna ofisa mmoja wa TFF pale, anakuwa ni mtu wa upande mmoja, anataka kutuuma sisi kwa kuwa yeye ni shabiki.

SALEHJEMBE:Shabiki kwa kuwa ametimiza uamuzi uliopitishwa?
Hans Poppe: Uamuzi haukuwa sahihi, fedha zetu zimechukuliwa. Sehemu tuliyoshinda sisi hatujapewa haki yetu. Huyu mtu ametuumiza sana na nilikutana na Malinzi (Rais wa TFF), nikamueleza.

SALEHJEMBE: Ukamueleza kuhusiana na nini, ulimtaja kiongozi huyo?
Hans Poppe: Ndiyo, nimemueleza aache kumkumbatia huyo mtu, atamjengea maadui maana anaharibu mambo mengi sana na hasa akijua yanahusiana na Simba.

SALEHJEMBE: Tukiachana na hilo, vipi kuhusu uwanja wenu maana kama mnazunguka tu?
Hans Poppe: Tunazunguka kivipi?

Championi: Hadithi, utaisha, sijui unakaribia lakini hakuna kitu.
Hans Poppe: Unajua watu hamuelewi, uwanja hauwezi kukamilika bila nyasi bandia. Ndiyo tulikuwa katika hatua za mwisho kuhangaika kuzitoa.

SALEHJEMBE: Mmefikia wapi?
Hans Poppe: Mwishoni, zikitoka ni suala la siku tano. Mtaalamu kutoka China amesema ni siku tano tu.

SALEHJEMBE: Mmebakiza hatua zipi?

Hans Poppe: Kutandika mabomba, ‘leya’ ya mwisho ya mchanga halafu kutandika kapeti, ni kama mvua zisipoendelea kunyesha na kuharibu hatua tuliyofikia.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV