March 3, 2017





Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba raia wa Romania tayari ameanza majukumu ikiwemo kukaa benchi baada ya awali kukosa kibali cha kufanya kazi na hivyo kulazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda.

Tangu aanze kazi rasmi ameshinda michezo miwili mfululizo, kwanza Azam iliifunga Mwadui mabao 2-0 katika Ligi Kuu Bara kisha kuichapa  Mtibwa Sugar bao 1-0 kwenye Kombe la FA.

Cioaba ambaye amewahi kuzifundisha klabu za Uarabuni na Afrika Kaskazini na Magharibi zikiwemo Raja Casablanca, Al-Masry, Al-Tadamun (zote akiwa msaidizi), Shabab Al-Ordon, Aduana Stars, Saham, Al-Oruba, Al-Shabab, Saham na Aduana Stars.
 

“Nahitaji muda wa kutosha ili kuwatambua vizuri wachezaji wangu, nazungumza na kila mmoja, nipo hapa kuipeleka Azam katika levo tofauti, kwa kuanzia nataka timu imalize ligi ikiwa ndani ya tatu bora,” anasema kocha huyo.

Uhaba wa kufunga mabao kikosini kwake
“Ni kweli na ninalitambua hilo, tayari nimeanza kulifanyia kazi mazoezini, naimani litakwisha.

“John Bocco mmoja kati ya wachezaji wazuri hapa Tanzania ingawa amekuwa na majeraha yanayomfanya kushindwa kucheza vizuri, kuna Yahaya Mohammed ambaye nilifanya naye kazi nchini Ghana msimu uliopita akimaliza kama mfungaji bora.

“Yahaya anahitaji maandalizi mazuri, nimezungumza naye kuhusiana na hilo pamoja na Bocco, Shabani Idd na Samuel Afful wanatakiwa kujua nini cha kufanya wakiwa ndani ya eneo la 18 na huo umekuwa ndiyo mpango wangu kwa wiki mbili sasa kabla ya mechi yetu ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbabane Swallos.

Kwa nini Enock Atta Agyei humtumii?
“Nashindwa kumtumia Agyei kwa sababu ana tatizo linalohusiana na vibali vyake vya kucheza, uongozi unalishughulikia, umeshapeleka maombi Fifa.

“Agyei ni mchezaji mzuri halafu bado kijana mdogo na anaweza kuwa tegemezi ndani ya timu hapo baadaye maana nilikuwa naye Ghana.

Kuhusu Mbabane Swallos 
“Kwa sasa mipango na akili  tumeelekeza katika mechi yetu ya ligi ambayo tutacheza Jumamosi hii (kesho) dhidi ya Stand United.

“Baada ya hapo nitakuwa na wiki moja ya kufanya maandalizi kabla ya mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa sababu naijua vizuri timu yenyewe kutoka Swaziland maana malengo yangu ni kucheza soka safi ambalo litaleta matokeo mazuri kwetu.

Uliwaona wapi Mbabane?
“Nawajua kwa sababu niliwatuma watu wawili kutoka kwenye benchi la ufundi  wiki mbili zilizopita kwenda Swaziland kuwaangalia katika mchezo ambao walishinda mabao 2-1 dhidi ya timu kutoka Botswana. 

“Licha ya hivyo nimeweza kupata kila kitu chao zikiwemo CD za mechi zao, nitazitumia katika maandalizi yangu kwa sababu soka linahitaji taarifa nyingi  kutoka kwa wapinzani wako kwani itatusaidia kupata pointi.

 Matarajio katika Kombe la Shirikisho yapoje?
Kikubwa ni kushinda mechi zetu zilizopo mbele, kitu ambacho kila mtu anahitaji katika kazi yake ingawa wakati mwingine unaweza kufungwa au matokeo ya sare.

“Malengo makubwa ni kufika mbali katika michuano hiyo kwa kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu hasa za nyumbani kwa kucheza kwa kushambulia muda wote maana soka lina matokeo ya makubwa ya kushangaza japo si vizuri sana kuongea kabla ya mchezo kwani hatujui nini kitatokea.

Makocha wa Hispania waliopita hawakufanikiwa, umejipangaje kurejesha makali ya Azam?
“Kama nilivyosema awali kwanza niliongea na kila mchezaji na kumueleza kama kocha nahitaji kitu gani nao kuweza kunielewa mimi.

“Nina wiki saba hapa ila timu inazidi kubadilika kadiri siku zinavyosonga kwa sababu naamini muda unavyokwenda nitakuwa na kikosi bora zaidi kwani naikubali kazi yangu.

“Tatizo ambalo naliona kubwa ni kuweza kuwawezesha wachezaji wangu waweze kujituma lazima kuwepo na huduma bora zaidi kwa wachezaji ikiwemo posho ya kutosha ambayo itarudisha morali kwa wachezaji pamoja na kupata sapoti kwa watu wote.

Unamzungumziaje Mkurugenzi wa Ufundi wa  Yanga, Hans Van De Pluijm?
NI kocha mzuri ambaye anaijua kazi yake kwa sababu tulikuwa wote Ghana tukifanya kazi katika timu tofauti, ingawa Ghana ni nchi nyingine na mipira wao ni tofauti na wa hapa kwa kuwa wao wana wachezaji bora na ambao wana tofautiana na wa hapa ambao ni bora lakini uwezo wao haulingani.

“Lakini yeye sasa ni mkurugenzi na mimi ni kocha ila tunajuana vizuri ingawa baada ya wiki mbili nitakutana na timu yake, kwangu mimi nahitaji matokeo mazuri pekee ndiyo kitu muhimu licha ya kwamba namuheshimu kwa sababu ni kocha  wa muda mrefu na mwenye uzoefu.

Viwanja vya mikoani ni tatizo labda wewe unazungumziaje?
“Kiukweli ni kitu cha kushangaza kwa sababu viwanja vingi havikidhi viwango ambavyo Azam tunaenda kucheza lakini Simba na Yanga wamekuwa wakipendelewa na shirikisho kwa kucheza kwenye Uwanja wa Taifa pekee mechi zao nyingi.

“Sasa kila mmoja anahitaji kucheza kwenye viwanja vizuri lazima watoe nafasi na kwa wengine watumie vyao ambavyo vipo sawa ili kila timu iweze kuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa, usiwe wa timu chache.

Vipi kuhusu bingwa wa ligi kwako upoje?
“Ubingwa bado naamini hauna mwenye licha ya Simba na Yanga kuwa na sapoti kubwa na niliangalia mechi yao Yanga walicheza vizuri kipindi cha kwanza na Simba wakacheza kipindi cha pili wakafanikiwa kuibuka na ushindi, zote ni nzuri naziheshimu.


“Kuhusu ubingwa hata sisi tunaweza kuchukua kwa sababu timu bado zimebakisha mechi nyingi na lolote linaweza kutokea upande wao na kwetu ukawa vizuri licha ya wao kuwa na tofauti kubwa ya pointi sita na sisi," anasema Cioaba.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic