March 18, 2017Unaweza kusema huu ni uzalendo, maana Shiza Kichuya ambaye yupo nafasi ya pili kwenye listi ya wafungaji bora msimu huu kwenye ligi kuu akiwa nayo 11, amesema kama akikosa nafasi yeye ya kuwa mfungaji bora basi angependa kuona Simon Msuva wa Yanga mwenye 12 akichukua kiatu hicho na siyo mchezaji kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya wachezaji wa kimataifa ambao wapo kwenye mbio za kuwania kiatu hicho ni Amissi Tambwe mwenye tisa, Donald Ngoma ana mabao nane sawa na Obrey Chirwa, wachezaji wote hawa wanachezea Yanga.

Kichuya ambaye anasifika kwa kasi pamoja na kufunga mabao kwa mashuti makali, amesema kwa jinsi upinzani ulivyo hivi sasa katika kuwania ufungaji bora kwa upande wake yupo radhi kiatu hicho kikatua kwa mpinzani wake ama mtu yeyote lakini hatafurahi akiona kinaenda kwa mchezaji kutoka nje ya nchi.

“Mimi nimeshasema tangu mwanzo atakayechukua kiatu ndiye aliyepangiwa na Mungu, ila naomba achukue wa hapa kwetu yeyote kati yetu na hata akichukua Msuva ni sawa tu.


“Nimejipanga kuhakikisha naisaidia timu yangu iweze kutwaa ubingwa msimu huu kwa kuhakikisha najituma mazoezini na kuifanya timu iweze kuwa vizuri zaidi na kuweza kufunga.

"Iwapo nitafanikiwa kufunga na kuchukua kiatu itakuwa sawa, kuhusu kufanikiwa kufunga Yanga mara mbili kwenye ligi msimu huu ni kutokana na kujituma tu mazoezini na hakuna siri yoyote,” alisema Kichuya.


1 COMMENTS:

  1. Very unprofessional indeed. Kama ni kweli huo ndio mtazamo wa Kichuya na mwandishi anayemwunga mkono kwamba ni mzalendo, basi soka letu lina safari ndefu sana kufikia kuwa la kulipwa. Sijapata kuona mawazo ya hovyo kama haya.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV