March 4, 2017Kuna utata kuhusu rufaa ya Yanga dhidi ya kadi nyekundu ya nyota wake Obrey Chirwa kwani kuna taarifa zinazosema Kamati ya Saa 72 itakutana leo na nyingine zinasema kesho.


Mwamuzi Ahmed Simba Jumatano wiki hii alimwonyesha kadi nyekundu Chirwa baada ya kumwonyesha kadi ya pili ya njano. Lakini lalamiko lilikuwepo katika kadi ya kwanza wakati mchezaji huyo alipopiga kichwa kuifungia Yanga bao dhidi ya Ruvu Shooting.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alithibitisha shirikisho hilo kupokea rufaa ya Yanga ambayo ilifuata taratibu zote ikiwemo kulipia Sh 300,000 na kilichobaki ni kamati kukutana.

“Yanga imeleta hapa kila kitu kuhusu rufaa yao na kuna uwezekano kesho (leo) kamati ikakutana kumaliza suala hili na hilo nina uhakika nalo wala hakuna tatizo,” alisema Lucas.


Hata hivyo, jana mchana Mwenyekiti wa Kamati ya Saa 72, Ahmad Yahya alisema rufaa ya Chirwa itakaliwa kikao keshokutwa Jumatatu pamoja na mambo mengine.


“Mechi ya Yanga imechezwa Jumatano jamani hivyo ni lazima tuipeleke hadi Jumatatu, ile ya Simba na Mkude mechi ilichezwa wikiendi na tukakutana wikiendi yake, hili neno saa 72 ni jina tu,” alisema Yahya.Endapo kamati hiyo haitakutana ni wazi Chirwa hatoichezea Yanga mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.  

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV