Kikosi cha Azam FC leo Jumamosi inacheza na Stand United kwenye uwanja wake wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam na habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kwamba John Bocco amereja.
Kocha Msaidizi wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wanautumia mchezo huo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand kama sehemu ya maandalizi yao ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland wikiendi ijayo.
Cheche alisema kikosi chake kipo vizuri kuelekea mchezo huo wa kimataifa ikiwa ni pamoja na kufanya vyema kwenye ligi ili kuweza kumaliza katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi.
“Tumejiandaa vizuri na mechi yetu dhidi ya Stand United, tunahitaji kushinda mchezo huo ambao tunautumia kujiandaa na mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Mbabane Swallows.
“Wachezaji wetu wote wapo vizuri na John Bocco amerejea rasmi kwani tulimchezesha dakika chache katika mechi iliyopita ili kuweza kuona kiwango chake, ila sasa yupo fiti kabisa,” alisema Cheche.
“Wachezaji wote wanaonyesha morali ya hali ya juu katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zote zilizobakia za ligi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment