March 17, 2017
Na Saleh Ally
ISSA Hayatou ameshindwa kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) baada ya kupata kura 20, Ahmad Ahmad akizoa 34 na kuwa rais mpya wa Caf. Huu ni ushindi mkuu mpya wa soka barani Afrika, “mbuyu umeanguka”.

Mwaka 2006 ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuripoti michuano mikubwa. Nilikuwa jijini Cairo, Misri kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, sasa wanaiita Afcon.
Kwa miji mikubwa zaidi ya Bara la Afrika, hadi wakati huo nilikuwa nikiujua wa Johannesburg, Afrika Kusini niliokwenda kikazi mwaka 2001 na baadaye 2004. Mwaka huo, nilishangazwa na ukubwa wa Cairo ambao ni kati ya miji mikubwa ya Afrika.

Huo ndiyo mwaka wangu wa kwanza kukutana ana kwa ana na Issa Hayatou, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), wakati huo.
Kukutana naye ana kwa ana ilikuwa utafikiri sijui umemuona nani, sijui ni mtukufu fulani. Mimi bila ya woga, kukiwa na rundo la waandishi, nikatupa swali langu lililozua tafrani kubwa.

Wakati wengine wameanza kuuliza kwa heshima na taadhima, mimi nilihoji kwa nini Caf wasifanye utaratibu mzuri, rais au kiongozi wa juu kama Hayatou asiongoze zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano mitano. Yaani miaka 10 iwe mwisho?

Hayatou alikuwa ameingia kuiongoza Caf mwaka 1988, akaendelea kubaki hadi wakati huo.

Ilionekana kama nimetenda dhambi kubwa kwa waandishi hasa kutoka Misri. Walianza kufoka kwa Kiarabu, sikuelewa lakini niliona waandishi kutoka Algeria wakibishana nao na ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kujua Algeria na Misri hawapatani.

AHMAD

Baada ya hapo, Hayatou hakuruhusiwa kujibu swali langu, sikuruhusiwa kuuliza maswali. Alizungumza kwa dakika sita tu, akaondoka zake!

Ajabu! Baada ya hapo, waandishi wote wakageukia kwangu hasa wale wanaotokea mashirika kama BBC, Reuters na wengine. Wakaanza kunihoji, nami bila ya woga, utafikiri Hayatou “mpya” nikajibu moja baada ya jingine ingawa mawimbi yalinitatiza kutokana na Kiingereza cha kuunga wakati huo.

Hayatou alikataa kujibu swali langu mwaka 2006, leo miaka 11 baadaye anaondolewa madarakani na kumbuka wakati huo tayari alikuwa amekaa madarakani kwa miaka 18.

Hata waseme nini, hasa viongozi wa mashirikisho ya soka barani Afrika, mfano Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mengine ya Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi na kwingineko, nitawaambia Hayatou alikuwa adui mkubwa wa soka la Afirka Mashariki.

Siku mzozo kati yangu na Hayatou unaibuka, baadaye niligundua aliishahama kwao Cameroon, alioa Misri na alikuwa ni mkazi wa Jiji la Cairo.

Unajua namna Waarabu wa Kaskazini mwa Afrika walivyougeuza mpira wa Afrika kuwa mali yao. Walikuwa wanafanya wanavyotaka, waamuzi waliwabeba wazi na viongozi wengi wa mashirikisho yetu waliendelea kuwa kama vibaraka, wapole, wasikivu, wasio na kauli kwa kuwa tu wanamsikiliza mkuu.

Ukiniambia Hayatou amesaidia mpira wa Waafrika, mimi nitakuambia sawa lakini kwao Cameroon, Afrika Magharibi kwa jumla pia ukweni kwake Misri na Afrika Kaskazini kwa mabwana zake ambao alikuwa anawaamini.

Nchi pekee ya Afrika hasa chini ya Jangwa la Sahara ambayo aliishindwa ni Afrika Kusini na kwa kuwa ina uwezo mkubwa wa kifedha na shirikisho lao lina uwezo mkubwa wa kifedha.

Hayatou alikuwa ana tabia kubwa ya kujikomba kwa mashirikisho yenye uwezo kama Nigeria lakini akaonyesha utiifu wa juu kwa Misri kwa kuwa wao ndiyo mashemeji zake.

Alikuwa Mwafrika mwenye huruma kipande kutokana na upande anaofaidika nao. Sasa ni zamu ya Ahmad naye kuona kuwa ukanda anaotokea umedorora kisoka.

Caf ya Hayatou ilijaa kashfa kuu ya rushwa na ubadhirifu kama ilivyokuwa kwa Fifa ya Sepp Blatter.

Huu ni wakati wa Ahmad naye kuonyesha njia sahihi lakini asikubali kuwa mtwana wa Misri, Waarabu wa Kaskazini na mabepari wa Magharibi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV