March 17, 2017Kama unamkumbu Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, leo Ijumaa anatarajiwa kuingia makubaliano ya kusaini mkataba wa kuifundisha Singida United.

Kocha huyo hivi karibuni alitimuliwa Yanga baada ya klabu hiyo kuyumba kiuchumi.

Singida United nayo ilipanda kucheza Ligi Kuu Bara kwenye msimu huu ikiwa chini ya Kocha Mkuu Felix Minziro aliyewahi kuwa kocha na mchezaji wa Yanga.

Taarifa zinasema kuwa Pluijm anatarajiwa kusaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho leo Ijumaa baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano mazuri.

Imeelezwa kuwa Pluijm tayari ameanza kufanya usajili wa wachezaji wapya watakaowatumia msimu ujao na kwa kuanza tayari amemsajili kiungo mchezeshaji wa Chicken Union ya Zimbabwe, Tafadzwa Kutinyu mwenye umri wa miaka 22 aliyekuwa anatajwa kwenye usajili wa Yanga kwa ajili ya kumrithi Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

"Pluijm analetwa Singida baada kusaidiwa na mmoja wa mawaziri wa hapa nchini ambaye amewezesha kocha huyo kukubali kuifundisha Singida United.

"Wakati akisubiria kusaini mkataba huo, kocha huyo tayari ameanza kufanya usajili kwa kumnasa mmoja wa viungo hatari na wanaochipukia hivi sasa Zimbabwe kutoka klabu ya Chicken Union ambaye ni Kutinyu," alisema mtoa taarifa.

Alipotafutwa Pluijm kuhusu hilo, alisema: "Sikia nikwambie kitu, wewe ni rafiki sana wa karibu, nikuthibitishie tu kuwa mimi kesho (leo) nataraajiwa kusaini mkataba na moja ya klabu hapa nchini lakini siyo Simba.

"Ningekutajia hiyo klabu lakini kutokana na makubaliano tuliyokubaliana ni kuwa sitakiwi kuzungumza lolote lile leo (jana) hadi hapo kesho (leo) nitakaposaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo na hivi sasa tupo kwenye mazungumzo ya mwisho."


Naye Mwenyekiti wa Singida United, Yusuph Mwandani, alipotafutwa alisema: "Timu yetu hivi sasa tumeifanya kuwa kama kampuni na kuna watu ambao wanaweza kulizungumzia hilo lakini siyo mimi, hivyo ni vema wakatafutwa wao.” 

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV