March 17, 2017Baada ya sakata la Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufungiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kudaiwa kiasi cha shilingi bilioni moja ambazo ni malimbikizo ya mshahara wa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo tangu mwaka 2010, imebainika kuwa klabu ya Yanga nayo inahusika katika kuiponza TFF mpaka kufungiwa.


Yanga inaingia kwenye deni hilo kutokana na makato ya mechi kati ya Yanga na TP Mazembe waliyocheza Juni 28, mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo mashabiki waliingia bure huku kukiwa hakuna makato yoyote yaliyopelekwa serikalini.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema kuwa deni ambalo wanadaiwa hivi sasa ni la kutoka mwaka 2010 kutoka kwenye uongozi uliopita ikijumlisha ujio wa timu ya Brazil, kodi ya mshahara wa Maximo pamoja na mechi ya mwaka jana kati ya Yanga na TP Mazembe kutokana na makato yake kutolipwa.


“Ujio wa timu ya Brazil mwaka 2010 ambayo ilikuwa ikienda Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia pamoja na makato ya Maximo ndiyo yamechangia kuwepo kwa deni ambalo halikuwa katika uongozi wa sasa lakini tunalazimika kubeba mzigo huo kwa kuwa taasisi ni ileile na kama ilivyokuwa ikijulikana kocha alikuwa akilipwa mamilioni ya fedha.


“Pia makato ya mechi kati ya Yanga na TP Mazembe ambapo mashabiki waliingia bure na kama inavyojulikana serikali haidili na klabu badala yake inadili na TFF,” alisema.


“Uongozi umeshafanya mazungumzo na TRA ambapo tumefanikiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni mia tatu na ofisi zimeshafunguliwa kwa hivi sasa.


Kwenye mchezo huo baina ya Yanga na TP Mazembe wa Kombe la Shirikisho, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji alitoa tamko kwa mashabiki wote waende kutazama mechi hiyo bila ya kulipa viingilio. Yanga walifungwa kwa bao 1-0. 


1 COMMENTS:

  1. Tusidanganyane, TRA inakata kodi kwenye mapato. So haiwezekani TRA idai kodi pasipo mapato!!TFF hawajielewi na hilo tayari TRA walitoa ufafanuzi

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV