March 11, 2017Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon, ametamka wazi kuwa wanaofikiria kikosi hicho kitapoteza mechi zake za Kanda ya Ziwa basi watakuwa wanajidanganya kwani wamepanga kuweka rekodi kwa msimu huu ya kutofungwa na timu yoyote ya huko.

Simba yenye pointi 55 ikiwa kileleni mwa ligi kuu, inatarajiwa kucheza na Kagera Sugar, Mbao na Toto Africans ambazo walizifunga kwenye michezo ya raundi ya kwanza, mechi zote zilichezwa kwenye Viwanja vya Uhuru na Taifa vilivyopo jijini Dar.


Katika michezo hiyo, waliichapa Kagera Sugar mabao 2-0, wakaibamiza Mbao 1-0 na kisha wakaimaliza Toto kwa mabao 3-0, hivyo sasa wanaenda kukutana nazo huko Kanda ya Ziwa.

Omog amesema pamoja na timu yake kuwa na kasumba ya kupoteza mechi za ukanda huo lakini safari hii wanataka kuweka rekodi wa kuhakikisha wanashinda kwa ajili ya kujiweka zaidi kwenye nafasi ya kutwaa ubingwa.


"Kila mechi sasa ni muhimu na hatutaki kuona tunapoteza hata pointi moja iwe ugenini au nyumbani na nina hakika tutafanya vizuri kwenye mechi hizo kwa sababu soka la kisasa haijalishi wapi unacheza, ukiwa bora tu unashinda.


"Tunataka kuvunja rekodi mbaya ya kufungwa, hasa Mwanza ambako tumekuwa tukipata matokeo mabaya kwa misimu kadhaa, lakini sasa tunataka iwe mwisho na hilo linawezekana kwa sababu tuna kikosi imara na kizuri kuliko wapinzani wetu," alisema Omog.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV