March 10, 2017
Na Saleh Ally
NIMEKUWA nikikumbushia mara kwa mara kuhusiana na suala la mashabiki wa klabu kongwe nchini kuonyesha mapenzi makubwa kuhusiana na klabu hizo.


Kila mara nimekuwa nikigawa makundi mawili ya mashabiki hao bila ya kujali ni mashabiki tu au ni wanachama. Hapa huwa nawajumlisha ni wale wanaozipenda klabu zao.
Ukisema klabu kongwe hapa nyumbani inajulikana ni Yanga na Simba. Zote makao makuu yake ni Kariakoo jijini Dar es Salaam.


Hakika Yanga na Simba zinapendwa sana tena sana. Kuna watu wako tayari hata kujitoa uhai, wako tayari kwenda jela na wengine wazikimbie familia au kukubali kutumia fedha ya chakula au ada ya shule kwa sababu ya timu za Simba na Yanga.


Ni klabu zinazounda timu zinazopendwa mno na mashabiki kuliko nyingine zote katika Ukanda wa Afrika Mashabiki.
Mimi nimekuwa nikiyagawa makundi ya wale wanaozipenda kweli kwa lengo la kuona zinapata mafanikio. Wako wanaosema wanaipenda Yanga au Simba kwa ajili ya maslahi yao binafsi, jambo ambalo ni sehemu ya sumu kali inayozisumbua timu hizo.


Kumekuwa na wanachama walio ndani ya Simba au Yanga, wamekuwa wakifaidika sana na mauzo ya wachezaji ndiyo maana unaona kila msimu kunakuwa na usajili wa mbwembwe sana hata kama hakuna sababu za msingi.
Karibu kila mchezaji anayejiunga na timu hizo, anakuwa ni mtaji wa wajanja fulani walio ndani ya klabu, iwe ni Simba au Yanga.


Mashabiki hao hujigeuza mbele ya watu wakitaka kuonekana ni watu wasio na ukaribu na wachezaji hao hata kidogo. 
Wao ndiyo wanaozizunguka klabu zao wakati wa usajili ili wapate “cha juu”.


Watu hao maarufu kama “Mtu wa Kati” wamekuwa wakienda mbali zaidi, kuwashawishi wachezaji wagome au kushinikiza mambo fulani. Inawezekana kwa kuwalaghai au kwa kuwaeleza ukweli.


Lengo linakuwa ni kila upande kati ya hizo mbili, yaani ile ya “Mtu wa Kati” na mchezaji zifaidike. Hapa kunakuwa hakuna maslahi ya klabu na yale mapenzi wanayoyaonyesha hadharani inakuwa ni uongo na unafiki mtupu.


Utaona wakati mchezaji anapokaribia kumaliza mkataba wake, kutakuwa na tabia fulani ambazo si za kawaida. Tabia ambazo zinaonyesha mchezaji amenuia kufanya jambo akipingana na klabu yake.


Angalia zile mbwembwe za kugoma au kuringa kama akina Donald Ngoma, Vicent Bossou kwa upande  wa Yanga. Au akina Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu kule Simba.


Kikubwa ni kuweka shinikizo ili kupata mkataba mnono. Hapa ni kuwapa presha viongozi na “Watu wa Kati” wanakuwa rafiki wa viongozi na wachezaji. Hivyo wanacheza “kati” kweli ili kuhakikisha wanafaidika na nyuso zao zikiwa na ulaghai wa juu.


Unaweza ukaona mambo ni magumu sana kwa klabu kwa kuwa haina maelewano na mchezaji au wachezaji fulani. Ajabu utaona wahusika wakilalama. Kumbe wao wanahusika na wanajua kila kinachoendelea lakini kikubwa wanachotaka kwanza ni kujifaidisha wao.


Hao ndiyo wanaowagawa wachezaji kutokana na kuwathamini zaidi ambao wanaona wataweza kuzifaidisha. Kwa utaratibu huu sasa unaanza kuona klabu ndiyo inakuwa inawafaidisha zaidi “Mtu wa Kati” ambao kwa taswira ya nje, wanajificha kwenye kimvuli cha kuonyesha mapenzi yao kwa Yanga hadi imekuwa wendawazimu.


Lazima tuwe wakweli, ndugu zangu “Mtu wa Kati”, muache tabia za kizamani zilizopitwa na wakati. Kutaka kuonekana kwenye jamii ya Wanasimba na Wanayanga kama watu wema na wenye mapenzi makubwa na klabu.

Kumbe mapenzi yenu ni malipo ya kujifaidisha matumbo na mifuko yenu kupitia klabu. Tena kitu kibaya zaidi, mchezaji ambaye mnamshawishi na mnafaidika naye mnamuona ni rafiki na mtu bora kwa kumtetea kila sehemu.Ikitokea akashituka kuhusiana na mifumo yenu. Mnaanza kutembea na kutembeza kampeni ya chinichini kutaka aonekane mbaya. Hii si sahihi na mnapaswa kuwa makini au kubadilika kwa kuwa dunia tuliyopo, si ya mwaka jana tena.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV