March 13, 2017



Na Saleh Ally
WIKI iliyopita niliandika makala kuhusiana na suala la kuondoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Hans van der Pluijm.

Yanga imevunja mkataba wake na Pluijm raia wa Uholanzi ambaye awali alikuwa kocha mkuu, halafu ikampandisha cheo na kumpa George Lwandamina raia wa Zambia.

Kati ya vitu vilivyokuwa vinanishangaza ni Yanga kuona Pluijm kama amefika mwisho halafu wakampandisha cheo na kumleta mtu mwingine ambaye walimuweka chini yake lakini wakiamini ndiye sahihi na bora kuliko yeye.

Baada ya hapo, kama nilivyoamini itakuwa, kulikuwa na mkorogano na vurugu za kila namna. Kila jambo lililotokea lilionekana kuwa lilisababisha na Pluijm au vingine vyovyote.

Mfano, mchezaji aliyegoma, ilielezwa ni Pluijm anaweza kuwa chanzo kwa kuwa ni rafiki yake. Aliyecheza vibaya ilielezwa inawezekana ni sababu ya Mholanzi huyo na kila kitu kibaya.

Hakuna aliyemsifia tena Pluijm baada ya Yanga kushinda au kufanya vizuri. Ndiyo maana alipoondoka nikasema ni vizuri aende ili iwe nafasi nzuri ya kuupima uwezo wa Lwandamina.

Kwamba bila ya Pluijm kuwa katika timu, Yanga imefanya lipi hasa. Inawezekana ni wakati mzuri kwa Lwandamina kukosa sababu ya utetezi na sasa kuangalia anafanya nini.

Lakini juzi, mashabiki wa Yanga wamemvamia Pluijm wakitaka arejee. Hii ni baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Zanaco huku wageni wakionekana wako bora zaidi ya Yanga.

Mashabiki nawajua, wanakwenda kwa hisia au mihemko, wakati mwingine huwa hawatulii na kutafakari mambo. Sasa naona Yanga ndiyo wamefanya jambo sahihi ili kuwe na kipimo sahihi kuhusiana na kocha wao.

Wakati Pluijm anakaa pembeni, Lwandamina ndiyo kaanza kazi nafikiri hana hata siku mbili au tatu. Tayari anaonekana hawezi kazi yake?

Kingine ambacho mashabiki wa Yanga wanapaswa kujua, Lwandamina ameingiza kikosi uwanjani wachezaji wakiwa wanadai mishahara yao na wakati wa mazoezi ya mwisho, walilijadili suala hilo na wamekubaliana kupambana katika mechi hiyo na baada ya hapo waendelee kudai.

Maana yake, kama watakakuwa hawajalipwa hadi katika mechi ya majaribio, basi uongozi wa Yanga ujue kutakuwa na tatizo na wanapaswa kupambana nalo mapema.

Lwandamina si malaika, anaweza kuwa anajua na akakosea. Lakini kumpa nafasi ya kufanya kazi yake kunaweza kuwa vizuri zaidi na muda ni jambo jema.

Yanga wanaweza wakawa wanamfunga kamba wenyewe halafu mwisho wakamlaumu kuwa hana kasi. Katika timu kocha ndiye mjanga namba moja linapotokea jambo. Lakini vizuri akapewa nafasi.

Yanga kuanza na kuendelea kumsaka Lwandamina katika kipindi hiki ni kujizuia wenyewe kwenda mbele. Lazima kuwe na umakini mkubwa na kuwe na kumbukumbu za nyuma kuhusiana na mambo kadhaa.

Mfano, wakati anaondoka Ernie Brandts na kuchukuliwa Pluijm, kulikuwa na lawama kibao. Mafanikio yake na Belekum Chelsea ya Ghana kulichangia Yanga imchukue na baada ya misimu mitatu ndiyo imefanikiwa kufanya vizuri Afrika kama ilivyotaka ikiwa ni baada ya kutolewa mapema mara mbili.

Tena kumbuka Pluijm aliondoka na kurejea. Maana yake kuna uwezekano wa kurejea tena kama ataondoka vizuri na pia Lwandamina akishindwa anaweza kwenda na siku nyingine kurejea.

Kama Pluijm alihitaji misimu kadhaa ili kufanya vizuri Afrika. Vipi Lwandamina aonekane anaweza ndani ya msimu minne wakati kuna mambo rundo kama mazingira, usajili na marekebisho ya kikosi.

Hata Zesco aliyofanikiwa nayo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hakuwa amekaa nayo msimu mmoja tu akafikia pale.

Ushabiki lazima uwe na uthibiti wa mihemko na tafakuri hasa kupitia uchambuzi wa mambo na kumbukumbu. Yasipokuwepo haya, basi ni sawa na kujifunga kamba mwenyewe kwa kuwa kocha wa Yanga kwa sasa ni Lwandamina na mwingine.



4 COMMENTS:

  1. Tatizo la Yanga washaona dalili za mwakani kuwa wahapahapa na Azam na Simba kuwakilisha. Plujin aende kwa sasa na Lwandamina afanye kazi hao midomo juu waanza kuchangia ili mishahara ipatikane. Wanamtaka Plujin wanajua mshahara wake? Wengi wao walizuia Yanga isikodishe nembo kwa Manji na ndio wauzaji wa jezi ambazo hazinufaishi club. Wajiulize wachezaji ambao hata ktk ligi walikuwa hawapangwi sasa wanapangwa. Wajiulize je kuna hela ya kuhimili fitna kama kukodi hotel na gari wao wenyewe au ndio kila kitu watafanyiwa na Zanaco?

    ReplyDelete
  2. Tatizo la Yanga washaona dalili za mwakani kuwa wahapahapa na Azam na Simba kuwakilisha. Plujin aende kwa sasa na Lwandamina afanye kazi hao midomo juu waanza kuchangia ili mishahara ipatikane. Wanamtaka Plujin wanajua mshahara wake? Wengi wao walizuia Yanga isikodishe nembo kwa Manji na ndio wauzaji wa jezi ambazo hazinufaishi club. Wajiulize wachezaji ambao hata ktk ligi walikuwa hawapangwi sasa wanapangwa. Wajiulize je kuna hela ya kuhimili fitna kama kukodi hotel na gari wao wenyewe au ndio kila kitu watafanyiwa na Zanaco?

    ReplyDelete
  3. 3. Nakubaliana na Babuu Mpole kuhusu hiki kipindi kigumu ambacho yanga ipo. Tatizo la msingi ni "fedha" za kuiendesha club. Achana na Plujim, hata angekuwa Sir Ferguson asingeweza kuifanya yanga ishinde bila uwepo wa manjifedha. Wanachama na washabiki tulionao ni kusubiri matokeo mazuri tu lakini hawana mchango wowote wa namna ya kuiendesha club bila manji, INAUMA SANA.

    ReplyDelete
  4. Nope. Tuache ushabiki pembeni. Kitendo cha Lwandamina kufanya sub za ajabu ni chanzo kingine cha sare. Halafu Chirwa mwanzo mwisho alikuwa anarukaruka tu. Kamusoko aliyekuwa anapambana kati anatolewa ili kuua timu. Anaingizwa kiungo wa pembeni ambaye hata hana uzoefu. Wapo Kaseke na Mwashiuya wenye uzoefu wa kutosha wangechukua nafasi ya Chirwa aliyekuwa anawatengenezea wazambia wenzake. Halafu unatoa hoja dhaifu, eti Lwandamina kaanza jana tu, unataka kutuambia mpaka hapo Hans ndiye alikuwa anafundisha mbinu na mfumo uwanjani? Kuwa mkweli bana, hiki kinachoendelea ni Lwandamina, nothing else!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic