March 25, 2017


Na Saleh Ally
WIKI hii hakutakuwa na utamu wa Premier League. Mambo yote yataanza katika wiki ya Aprili Mosi kuelekea safari ya mechi za mwisho kabisa.


Zitakuwa ni tisa, kumi au 11 kulingana na timu zilivyocheza. Ubingwa nafasi zaidi iko kwa Chelsea pia angalau Tottenham wanaonekana kuwa na mwendo mzuri kama hawatateleza.

Manchester United ilikuwa ikizungumziwa kwenye ubingwa kila ulipofikia wakati huu. Lakini imepotea kwa takriban misimu minne mfululizo.

Msimu huu inaonekana kuwa na nafuu kubwa ingawa mwanzoni ilibezwa. Kutoka kuwa “mmiliki” wa nafasi ya saba, baadaye ya sita na sasa wako nafasi ya tano wakiwa wanafukuzia kuingia nafasi ya Top Four.


Takriban mwezi na nusu sasa, nilisema Man United wana nafasi kubwa ya kuingia Top Four, zaidi nikichambua aina ya uchezaji wao, wanafunga mabao machache lakini wagumu kupoteza.


Sasa wana pointi 52 katika nafasi ya 5, Liverpool ina 56 ikiwa ndani ya Top Four lakini utaona Man United wamecheza mechi 27 na Liverpool wana 29.


Kama Man United itacheza mechi zote mbili na kushinda, maana yake itafikisha pointi 58 na kuipiku Liverpool. Kama itakuwa hivyo basi kuna haja ya kusema wakati wa kurejea Top Four utakuwa umewadia na inawezekana kutoka itakuwa si kazi rahisi tena na unaweza kushangazwa nao ukisikia wako katika nafasi ya pili.


Mechi zao zinaweza kuwa mwamuzi mkubwa ingawa utaona sasa nafasi ya nne katika Top Four inawaniwa na timu tatu ambazo ni Liverpool inayoshikilia nafasi hiyo, Man United na Arsenal ambao wanaonekana kuwa ni ‘wataalamu’ wa nafasi hiyo ambao wako katika nafasi ya 6 wakiwa na pointi 50, pia wakiwa wamecheza mechi 27.


Ukiangalia kama Arsenal ni wa kuaminika, basi nao wakishinda mechi zao mbili, watawafikia Liverpool. Hata wakiwa chini yao, wanaweza kuendesha presha kuzidi kuwa kubwa lakini mwendo wao hauaminiki na si timu inayoweza kupanga jambo na kulitekeleza kwa kutimiza ndoto.


Nilishawahi kueleza kati ya Liverpool au Arsenal ni lazima moja iondoke kwenye Top Four, wakati huo Tottenham ilionekana haina nafasi na Man City ilikuwa ikiyumba ile mbaya. Sasa hali halisi inaanza kujitokeza.


Mechi nne zijazo za Man United zitakazoanza Aprili Mosi hadi Aprili 15. Ni siku za presha na mateso makubwa ya kutaka kubadili mambo lakini zitakuwa mwamuzi sahihi wa nafasi ya Man United kurejea Top Four au la.


Man itacheza dhidi ya Wes Brom, Everton, Sunderland na Chelsea. Inawezekana kabla ya kuivaa Chelsea Aprili 15, ikawa imefikia mwafaka kuwa imerejea au la na hakuna mechi laini lakini Man United wanaonekana kuanza kujitambua kweli.

Kwa Liverpool, huenda ndiyo wenye presha ya juu zaidi wakiwa na michezo miwili zaidi na wana uhakika wa kushushwa nje ya Top Four kulingana na hali halisi.


Mechi zao nne kuanzia Aprili Mosi ni dhidi ya Everton, Bournemouth, Stoke City na Wes Brom. Pia hakuna mechi laini hapa na utaona namna presha itakavyozidi kupanda kwao hasa kama watakosea katika mechi moja tu.


Unaweza kuona kama Arsenal nao wana nafasi kubwa lakini shida ni kuwa hawaaminiki, kwamba wana uwezo hata wa kushinda mechi nne mfululizo. Wakiweza hivyo, huenda wakatibua plani ya Man United na Liverpool.


Mechi zao ni ngumu pia, ndani yake wanakutana na moja ya timu zilizo Top Four ambayo ni Man City halafu West Ham, Crystal Palace na Middlesbrough, nyingi zikiwa ni zenye presha ambazo hucheza kwa kujituma kweli.


Zitakuwa ni siku 15 za presha na mwamuzi wa kile nilichokisema. Mechi hizo ndizo zitatoa picha ya mwisho kuhusu Man United kuwa wanarejea Top Four au wamefeli.
Man United pekee ndiyo wamekuwa wakipanda lakini kwa Arsenal na Liverpool kwa mujibu wa msimamo, wamekuwa wakiporomoka kila siku zinavyosonga mbele. Man United wakishikilia hivyo, maana yake wana uhakika wa kuingia Top Four na kumiliki nafasi moja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV