April 8, 2017Straika wa Simba, Ibrahim Ajibu amefunguka juu ya kuhusishwa na kujiunga na Yanga katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara akisema, hajui lolote kuhusu madai hayo na ataweka wazi kila kitu atakapomaliza mkataba wake.


Licha ya kupewa mkataba mpya na Simba, Ajibu bado hajausaini akisisitiza atafanya jambo hilo baada ya kumalizika kwa ligi ambapo pia mkataba wake na klabu hiyo utakuwa umefikia tamati.

Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za Yanga kumuweka Ajibu katika mipango yao ya msimu ujao huku wakitajwa kuwa chanzo cha mshambuliaji huyo kutosaini mkataba wa Simba.

Ajibu amesema: “Mimi sijui chochote juu ya madai ya Yanga kunihitaji nimekuwa nikisikia tu, na siwezi kusema lolote hadi mkataba wangu utakapoisha.


“Ninachokiangalia hivi sasa ni kuona ni jinsi gani naisaidia timu yangu kwani lengo letu ni kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu kwa kuhakikisha tunashinda mechi zote zilizobakia,” alisema Ajibu.


Mkataba wa kiungo huyo mwenye mabao sita kwenye ligi na klabu yake ya Simba unafika ukingoni mara baada ya msimu kumalizika ambapo pia taarifa zinasema anaweza kutimkia nchini Afrika Kusini.

Mbali na Ajibu kupewa mkataba kisha kutosaini, mchezaji mwingine wa timu hiyo aliye katika mazingira kama hayo ni nahodha Jonas Mkude lakini uongozi wa Simba umesema una uhakika wachezaji hao watabaki klabuni kwao.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV