April 8, 2017
Na Saleh Ally
KOCHA Zinedine Zidane wa Real Madrid atakuwa anafikisha mechi ya 300 leo akiwa na kikosi hicho wakati timu yake itakapoikaribisha Atletico Madrid katika mechi ya La Liga, kila upande ukiamini ni muhimu kwake.


Zidane ameitumikia Madrid kama mchezaji kwa mechi 227 na akiwa kocha mechi 73. Lakini inawezekana yote hayo asiangalie zaidi ya kutaka ushindi katika mechi hiyo maarufu kama Madrid Derby kwa kuwa ndiyo mechi inayowakutanisha vigogo wa jiji kubwa zaidi nchini Hispania.

Kimahesabu, Madrid wanataka kushinda ili kujihakikishia kubaki kileleni kwa kuwa wana pointi 71, lakini wapinzani wao wakubwa katika La Liga, FC Barcelona tayari wamekusanya pointi 69. Maana yake kama watapoteza wataendelea kubaki kileleni lakini wakiiba nafasi Barcelona kuwavuka kama wakiyumba tena.


PRESHA:
Kama hiyo haitoshi, kwa Madrid, mechi hiyo ina presha kubwa zaidi kwa kuwa Atletico ndiyo wapinzani wao wakuu unapozungumzia soka katika Jiji la Madrid.
Pamoja na kwamba kuna timu nyingine, vigogo wa jiji hilo ni timu hizo mbili na viwanja vyao vikiwa tofauti ya umbali kama kilomita 10 tu kutoka kila mmoja alipo.

Kawaida wanapokutana, jiji hilo linalazimika kuwa na ulinzi mkali kuhakikisha usalama unakuwepo wa kutosha kwa kuwa chuki kwa pande hizo mbili ni kubwa sana.WENYE MJI:
Madrid wamekuwa wakiamini wao ndiyo wenye jiji, wanajiita “Watoto wa Mjini” ukilingamisha na wenzao ambao wanaaminika ni watoto kutoka “nje ya mji” na wakati mwingine wamekuwa wakiwabandika jina la “Wavamizi”.Kuonyesha kila upande ni jeshi linalojitegemea wamejichagulia maeneo maalum ya kushangilia ambayo umbali wake ni kama mita 200 tu kwa maana ya tofauti na siku ya leo kuanzia asubuhi, eneo hilo linakuwa na ulinzi mkali kuhakikisha usalama.Mashabiki wenye jezi nyekundu na nyeupe, hawaruhusiwi kwenda upande wa sanamu la Cibele ambalo Real Madrid hukaa pale na kushangilia kabla na baada ya mechi. Sanamu hilo liko mbele ya makao makuu ya ofisi ya Manispaa ya Jiji la Madrid na ndiyo ofisi ya Meya wa jiji hilo, ndiyo maana Madrid wanajiita wenye mji.Atletico wao husherekea mbele ya sanamu jingine la Neptuno, ambako mashabiki wenye jezi nyeupe na zambarau au dhahabu, pia hawatakiwi kuvuka na kufika upande huo maana maafa yanaweza kuwakuta na haitakuwa lawama ya watu wa usalama.

Uwanja wa Santiago Bernabeu uko katikati ya Jiji la Madrid, na kikubwa ni ulinzi wa kutosha kuhakikisha kila upande unaingia na kutoka kwa usalama. Askari wanakuwa wakali sana kwa wanaotaka kuharibu mambo.

MAKOCHA:
Ukiachana na mashabiki, tayari Kocha Diego Simeone raia wa Argentina ameeleza namna mchezo utakavyokuwa mgumu akiamini Madrid ambayo iliwapumzisha BBC (Gareth Bale, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo) katika mechi iliyopita itawatumia na kutakuwa na kazi ngumu.

Simeone amesema wamejiandaa kupambana na presha kubwa katika dakika 20 au 25 za mwanzo kwa kuwa wanajua Madrid watahakikisha wanasukuma mashambulizi ya mtindo wa nyuki.

Hata hivyo, akasisitiza kwamba angependa kumuona mshambuliaji wake Antoine Griezmann anakuwa katika kiwango bora kwa kuwa ni mtu anayeweza kuamua mchezo.

Zidane anaonekana anajiamini lakini naye anakubali kwamba mchezo utakuwa mkali na mgumu na lazima wajiandae kwa kuwa wanataka kushinda zaidi ya Atletico.

TAKWIMU:
Mechi sita:
Ukiangalia mechi sita zilizopita zinaonyesha timu hizi zina mwendo mzuri unaofanana. Zote zimeshinda mechi tano na kupoteza moja.

Madrid walipoteza mechi yao dhidi ya Valencia wakati Atletico walifungwa na Barcelona. Hii inaonyesha timu hizo ziko fiti hali inayofanya mechi yao kuwa nguvu zaidi.

UBABE:
Rekodi zinaonyesha Madrid ndiyo wababe zaidi zinapokutana timu hizo ingawa hilo haliwezi kuwa mwamuzi wa dakika 90 za leo.

Katika mara 42 zilizokutana, Madrid imeshinda mara 25 na Atletico imeshinda mara 7 tu huku kukiwa na sare 10.

Pamoja na Madrid kuamini ni wababe, hii haijawahi kuwakatisha tamaa Atletico ambao wanaamini wao ndiyo kiboko cha vigogo hao.

Mabao:
Katika La Liga, Real Madrid hadi sasa imefunga mabao 78 na kufungwa 30 na Atletico 55 na kuruhusu 23 na kuifanya kuwa moja ya timu zenye difensi ngumu zaidi.

Hii maana yake ni hivi, zinakutana timu mbili, moja ikiwa na safu kali ya ushambulizi na nyingine ikiwa na difensi ngumu zaidi. Hapa matokeo yanakuwa magumu kuyabashiri kwa urahisi kwa kuwa atakayeteleza kuitumia silaha yake vizuri basi ndiye anayeanguka. Kila mmoja akiitumia vizuri, asilimia ya sare inapanda hadi kufikia 80.

Kitu kizuri zaidi kwa Simeone kikosi chake hakijawahi kuwa na hofu dhidi ya Madrid na kama alivyoeleza mwanzo, wanaweza kujilinda lakini baadaye wanashambulia kwa nguvu na kuwapa wakati mgumu.

Lazima itakuwa ni mechi ya presha na BBC watakuwa na wakati mgumu dhidi ya ukuta utakaoongozwa na  mtu kama Diego Godin na Gabi lakini Madrid lazima wafanye kazi ya ziada kuwazuia watu kama Angel Correa, Yannick Carrasco.


Inakuwa ni mechi moja inayojumuisha mengi, makocha wakitaka kuweka rekodi vizuri na kufikia mafanikio, hali kadhalika kwa wachezaji.


Kwa mashabiki, wao ni rekodi, ubabe na kuonyeshana lakini kutimiza furaha ya mioyo yao kwa kuwa kila mmoja anaamini ni bora zaidi ya mwenzake hata kama wote wanatokea kwenye jiji moja.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV