April 3, 2017





Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali, amesema straika wa timu hiyo, Mzambia, Obrey Chirwa, ameshindikana kwa jinsi anavyowanyanyasa wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara.

Mzee Akilimali ametoa kauli hiyo baada ya juzi Jumamosi Chirwa kuifungia timu yake bao pekee kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar.

Awali, wakati Chirwa aliposajiliwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, Mzee Akilimali alikosa imani na Mzambia huyo na kuanza kumuona ‘galasa’ baada ya kuanza vibaya katika ligi.

Lakini baada ya kuanza kuzifumania nyavu na sasa akifikisha mabao tisa, Akilimali amekuwa akimsifia kila kukicha na kusema ni miongoni mwa washambuliaji hatari na walioshindikana katika Ligi ya Bongo.

Mzee Akilimali amesema: “Kwa jinsi kiwango chake cha sasa kilivyo, hakuna neno rahisi la kulitamka zaidi ya kusema Chirwa ameshindikana, mwanzo sikuwa na imani naye kutokana na alivyoanza, lakini tangu nimbariki kwa kumvulia kofia, amekuwa haniangushi.

“Wachezaji wa aina hii ndiyo tunaowataka ndani ya Yanga, tukiwa nao wengi kama hawa nadhani tutafika mbali sana.”

Ikumbukwe kuwa, Oktoba 12, mwaka jana katika Uwanja wa Uhuru, Dar, Chirwa ndio alifunga bao lake la kwanza la ligi tangu ajiunge na Yanga walipoichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1 zikiwa zimepita mechi sita bila ya kufunga.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic