April 3, 2017Baada ya kiungo wa Yanga, Justine Zulu raia wa Zambia kupata jeraha la ugoko, daktari aliyemtibu, Nassor Matuzya amefunguka kuwa kiungo huyo atakaa nje ya uwanja kwa siku saba hali ambayo inaweza kumfanya kuukosa mchezo ujao dhidi ya Waarabu wa Algeria, MC Alger.

Zulu alipata majeraha hayo katika mchezo wa juzi Jumamosi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam baada ya kugongwa na kiungo wa Azam, Himid Mao, dakika ya 58 na kushindwa kuendelea na mchezo huo huku nafasi yake ikichukuliwa na Emmanuel Martin.

Matuzya aliwahi kuwa daktari wa Yanga, kwa sasa ni Katibu wa Chama cha Madaktari wa Tiba za Michezo Tanzania (Tasma) na pia ni daktari mkuu wa michezo katika Uwanja wa Taifa.

Ikumbukwe kuwa, Jumamosi ijayo, Yanga itapambana na MC Alger katika mchezo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa ambapo Zulu ameingia kwenye orodha ya majeruhi wa Yanga ambayo ni Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Amissi Tambwe.

Matuzya amesema kuwa, Zulu alipata michubuko miwili katika sehemu moja ya ugoko iliyotokana na kukwaruzwa na kiatu cha Himid.

“Palepale uwanjani tulimshona nyuzi kumi na tunatarajia atakaa nje ya uwanja kwa takribani siku saba akiwa chini ya uangalizi maalum.

“Lakini ndani ya siku hizo, itamchukua kama siku tatu kabla ya kutolewa nyuzi ili aanze mazoezi mepesi, lakini jambo la kushukuru ni kwamba licha ya jeraha lenyewe kuwa kubwa, kitendo cha kumuwahi kimesaidia kupatikana kwa unafuu.

“Alikuwa amevaa kizuia ugoko, lakini ukiangalia Himid alimkwaruza na hajamkita, hivyo kiatu chake kimemchana kwa umbali wa sentimita nne na nusu mpaka sita, na kama isingekuwa amevaa kabisa kizuia ugoko, basi jeraha lingekuwa kubwa sana,” alisema Matuzya.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV