Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, anaamini kabisa kama timu yake inataka kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ni lazima leo Jumamosi iifunge Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga na Azam tangu mwaka 2008, zimekutana mara 17 katika ligi kuu na zote zimeshinda mechi tano kila moja na zimetoka sare mara saba. Yanga imefunga mabao 23 na Azam imefunga mabao 22.
Katika msimamo wa ligi kuu, Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 53 nyuma ya Simba iliyo kileleni na pointi 55, Azam ni ya tatu na pointi 44.
Niyonzima raia wa Rwanda, amesema mchezo huo utakuwa mgumu kulingana na historia yao kila wanapo-kutana lakini kwao ni muhimu kwani wakishinda watakuwa na mwanga mzuri wa kutwaa ubingwa.
“Mechi yetu na Azam ni mchezo mkubwa na utakuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na kila upande kuhitaji ushindi, lakini tumejipanga kushinda kwani ndiyo mechi ambayo itatoa mwelekeo wa kutetea ubingwa wetu.
“Ni lazima tushinde mechi hii ili tujiweke katika nafasi ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, tuna majeruhi wengi lakini tutapambana ili tushinde,” alisema Niyonzima.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment