Leo Jumamosi Azam FC inacheza na Yanga katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bila ya straika wake John Bocco, lakini nahodha msaidizi wa timu hiyo, Himid Mao amepiga mkwara kwa kusema ni lazima washinde.
Bocco ambaye ni nahodha wa Azam anasumbuliwa na goti na hatokuwepo katika mchezo huo namba 169 utakaochezeshwa na mwamuzi Jonesia Rukyaa.
Mchezo huo una faida zaidi kwa Yanga endapo itashinda kwani ina pointi 53 nyuma ya Simba yenye pointi 55 huku Azam ikiwanazo 44 tu.
Mao amesema maandalizi ya kikosi chao kuelekea mchezo huo yanaendelea vizuri na wana imani kubwa ya kushinda licha ya kumkosa Bocco.
“Tumejiandaa kucheza na Yanga, kutokuwepo kwa Bocco hakuwezi kututisha kwani tutapambana kupata ushindi kwa sababu kuna mechi hakuwepo na tukapata matokeo mazuri,” alisema Mao.
Meneja wa Azam, Philip Allando, alithibitisha Bocco hatoweza kucheza mchezo huo kutokana na kutokuwa fiti akiandamwa na majeraha ya nyama za paja na goti. Hata hivyo, Bocco ameshaanza mazoezi mepesi.
Hii ni mechi ya 18 kati ya Azam na Yanga tangu mwaka 2008, ambapo timu zote zimeshinda mechi tano na kutoka sare mara saba.
0 COMMENTS:
Post a Comment