April 1, 2017
Kiungo Thabani Sikala Kamusoko wa Yanga ana asilimia 50 ya kucheza mechi ya leo dhidi ya Azam FC, lakini wachezaji wenzake Amissi Tambwe na Hassan Kessy wamemlazimisha kucheza mechi hiyo.

Yanga inacheza na Azam leo Jumamosi mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar s Salaam.

Kuumia kwa Kamusoko ambaye alishindwa kumaliza mazoezi jana kumeongeza idadi ya majeruhi kufikia watatu katika kikosi cha Yanga wengine wakiwa ni Donald Ngoma na Tambwe wote wakisumbuliwa na magoti.

Pia Kessy na Kelvin Yondani nao hawatacheza mechi ya leo kwani wanatumikia adhabu ya kukosa mechi kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Katika mazoezi ya Yanga jana asubuhi kwenye Uwanja wa Taifa, Tambwe alisikika akimwambia Kamusoko kuwa; “Ni lazima ucheze kwani hii ni mechi muhimu kwetu, jikaze na ujitahidi ucheze.
“Ujue tunapokosekana nusu ya wachezaji tuliokuwepo kwenye kikosi cha kwanza ni tatizo, binafsi nilitamani sana kucheza mechi hii lakini goti linaniuma sana.”

Kessy na yeye alisikika akimueleza Kamusoko; “Fanya vyovyote uwezavyo ucheze hii mechi, Azam wazuri kwenye kiungo, hivyo unapokosekana wewe ni tatizo kwenye timu.”
Tambwe aliliambia Championi Jumamosi kuwa: “Imetubidi kumlazimisha na kumpa moyo Kamusoko acheze mechi hii, kukosekana kwake kunaweza kuwa hatari kwetu.”

Akizungumzia hali hiyo, Kamusoko raia wa Zimbabwe alisema: “Najisikia maumivu, nimewaambia wachezaji wenzangu waniombee kwa Mungu ili niamke vizuri kesho (leo) ili niweze kucheza.”

Daktari wa Yanga, Edward Bavu akizungumzia afya ya Kamusoko alisema, kucheza kwa kiungo huyo ni nusu kwa nusu na jana jioni alitarajia kumfanyia uchunguzi wa mwisho.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV