April 7, 2017MAHADHI


Na Saleh Ally
KATI ya wachezaji ambao nilikuwa nina matumaini nao makubwa ni Juma Mahadhi ambaye amejiunga na Yanga akitokea Coastal Union ya Tanga.

Mahadhi ni mchezaji mwenye aina ambayo unaiona ina nafasi ya kufanya vizuri katika sehemu sahihi kutokana na kipaji alichonacho.

Mahadhi ana kasi, ana uwezo wa kupiga mashuti lakini ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira hali ambayo inaashiria ni mmoja wa vipaji bora vya baadaye Yanga.

Tangu ametua Yanga, kamwe hauwezi kuwalaumu kwamba hawakumpa nafasi kucheza kama ambavyo imekuwa kwa vijana wengine misimu miwili iliyopita.

Hata kabla ya kuondoka kwa Hans van Der Pluijm pale Yanga ambaye ndiye alimsajili Mahadhi, alikuwa akimpa nafasi ya kutosha kucheza licha ya kwamba amejaza rundo la wakongwe au wazoefu ambao wangechangia kinda huyo kupewa nafasi.

Baada ya ujio wa George Lwandamina, naye hakunyima nafasi kinda huyo, umeona ambavyo ametoa nafasi kadhaa tena wakati mwingine akimuanzisha.

Katika mechi alizoanzishwa, Mahadhi ameshindwa kuonyesha ushawishi kwamba ni mchezaji anayestahili nafasi hiyo na badala yake akamuacha kocha huyo na zile hisia, walio nje ndiyo sahihi zaidi.

Tangu ameanza kupewa nafasi ya kucheza, Mahadhi hajawahi kuonyesha kuwa kama Yanga itamkosa mechi ijayo au mechi tatu zijazo ni tatizo au kama Yanga itamkosa msimu ujao, basi itakuwa ni tatizo.

Badala yake inaonyesha kuwa Mahadhi ni mchezaji sahihi wa benchi ambalo si jambo sahihi kwa mchezaji sahihi na bora ambaye anataka kujiendeleza kupitia nafasi anayopewa.


Kawaida unaweza ukawa bora lakini usipate nafasi ya kuonyesha ulichonacho. Niliwahi kuelezea namna Emmanuel Martin aliyejiunga na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar anavyoitumia nafasi aliyopewa.

Mahadhi ni tofauti, sitaki kuwa watu wanaojenga msingi wa lawama kumlaumu, badala yake nataka kumkumbusha mambo kadhaa muhimu.

Mfumo wa Yanga ni timu inayotaka mafanikio ya haraka na inavyokwenda ni ile inaamini wako wenye uwezo wa kuipa mafanikio ya haraka zaidi. Ingekuwa Simba, huenda wangeendelea kumpa nafasi tena na tena na tena ili kuhakikisha anakua kimchezo.

Kila timu inakuwa na aina yake ya ukuzaji wa wachezaji au aina ya mchezo. Kuna utamaduni wa uwanjani na nje ya uwanja ambao unaweza kuutafsiri kama utamaduni wa timu na utamaduni wa klabu.

Kwa maana ya utamaduni wa timu, Yanga wanataka watu wanaowapatia wanachotaka kwa wakati mwafaka. Nafikiri Mahadhi ana kila sababu ya kuliangalia hilo mara mbili.

Tena haitakuwa vibaya kama ataamua kufanya kazi mara mbili zaidi ya wengine lakini kutumia juhudi na ujuzi kwa kila nafasi moja anayoipata kwa ajili ya kucheza.

Lazima ajue, nafasi anayoipata kuichezea Yanga ni sawa na bango la matangazo kwa mtangaza biashara. Kama alikuwa ana kiu basi anapaswa kuionyesha na kumpa kocha matumaini kama atamtumia.
Narudia mara nyingine kwa Mahadhi kwamba namuona ni mmoja wa wachezaji bora na hazina kubwa katika kikosi cha Yanga lakini ni hazina ya baadaye ya taifa.

Anapaswa kuonyesha uwezo sasa ili ategemewe na Yanga hadi katika michuano ya kimataifa na iwe ndiyo njia yake ya kutoka.

Mbwana Samatta anaonekana anapaa, ni kwa kuwa aliondoka kwa wakati mwafaka. Kama Mahadhi atang’ara sasa, ndiyo wakati wa kuaminiwa na Yanga na kuonekana kwa wengine.

Kama hatang’ara sasa, maana yake asubiri kuanza kung’ara akiwa na miaka 28 na mwisho wake utakuwa Dar es Salaam na kitakachofuata hapo ni “rivasi”.


Sitaki kuwa kwenye kundi la kumkatisha tamaa kwa kuwa kipaji anacho. Lakini mafanikio yatanatafutwa binafsi kupitia juhudi na maarifa.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV