April 3, 2017





Na Saleh Ally
INAWEZEKANA kabisa leo nitakuwa ninakumbusha mara nyingine tena baada ya mara nyingi nyingine nilizowahi kulizungumzia suala hili, lakini lengo ni kuleta mabadiliko.


Nimebahatika kusafiri nchi nyingi sana duniani katika mabara tofauti na nimejionea mengi ambayo nayachukuliwa kama mafunzo katika maisha yangu.


Nitakachokizungumzia hakitajali kuwa nimeona nchi jirani ya Kenya, mbali zaidi kama Afrika Kusini au Hispania na Ujerumani au Oman na Uturuki. Nimeona vitu vingi vinavyofanana lakini hapa nyumbani naona kila kitu kipo nyuma.


Kwanza nianze kwa kuipongeza Benki ya NMB ambayo imeonyesha mfano, imeingia kuidhamini timu ya Azam FC ambayo ni moja ya timu bora za Ligi Kuu Tanzania Bara. Kabla, NMB ilikuwa mdhamini wa timu ya taifa, Taifa Stars, kipindi ambacho hamasa iliamka na kuwa juu kweli.


Mpira wa Tanzania unaonekana kubadilika kwa kuwa kuna wadhamini kadhaa wamejitokeza na kudhamini. Hata michezo mingine imeanza kupata mwamko, mfano Multichoice Tanzania ambao walimdhamini Alphonce Simbu ambaye alishinda medali ya dhahabu katika Mumbai Marathon.


Hapa ninalenga mabenki, ninalenga makampuni mengi ya simu ambayo yanaonekana hayana msaada wowote na Watanzania hasa katika suala la udhamini katika sehemu ambako ni furaha na sifa ya Taifa.


Pongezi kwa Vodacom na Airtel ambao wameingia katika soka. Najua bado wana nafasi ya kuingia katika michezo mingine. Pia pongezi kwa TBL ambao hata kama waliondoka lakini walifanya vema katika soka na riadha ambako wanaendelea na Kilimanjaro Marathon.


Ninaamini kuna mabenki mengi, makampuni mbalimbali makubwa ambayo yanaweza kuingia kwenye michezo na kufaidika.


Siamini mabenki makubwa ya nchi mbalimbali hata zile za jirani nje ya Afrika wanapata faida wao watashindwa. Mara nyingi nimekuwa nikiamini kabisa, makampuni makubwa wamekuwa hawana ubunifu wa kutosha.

Wanakosa ubunifu wa kutosha kwa kuwa watu wao wa masoko wengi si wabunifu, watu wao wa masoko ni watu waliosoma Ulaya na wangependa mambo mengi yaende kwa mazingira ya Kiulaya.

Au inawezekana kabisa, wanaopewa nafasi hizo ni wale wanaozungumza Kingereza kizuri. Pia inawezekana kabisa wanaona wanachopata ni sahihi wakati wangeweza kupata zaidi.

Kuna haja ya kuangalia soko la Tanzania linataka nini na mimi, ninaamini michezo inaweza kubadilisha mambo, inaweza kutangaza zaidi na tayari tumevuka kule kwenye kusema kuna migogoro mingi na fedha zitaliwa.

Kuna haja ya kuangalia hata mikataba mifupi na kupima kinachodhaminiwa. Sisemi kwenye soka pekee, michezo mingi imelala kwa kukosa wadhamini wakati wadhamini wenyewe wakiendelea kudhamini pati za ukumbini kwa matakwa au furaha ya maofisa masoko wao.


Lazima tukubali kwamba fedha wanazopata mabenki ndiyo hizo za Watanzania. Wakati ni vizuri kuzirudisha na michezo ni sehemu ya furaha ya karibia watu wote kama ilivyo kwa muziki.

Michezo haiwezi kuendelea huku wenye uwezo wa kusaidia wakiwa kimya tu. Kupata kwenye jamii husika wakati mwingine vizuri kuwarudishia kwa njia ya kuwafurahisha huku ukifaidika.


Mechi za soka zinaangaliwa sana, wakati mwingine watu wanakwenda uwanjani na inakuwa rahisi kusikika au kuandikika. Jitokezeni, muonyeshe ubunifu na kwa maofisa masoko isiwe kwa ajili ya matakwa au faida zenu binafsi.


Angalia mfano wa mchezo wa soka, ndiyo unaopendwa zaidi duniani. Ndiyo unaopendwa zaidi Tanzania, vipi wadhamini hawaonekani. Kama mnapenda kwenda kwenye kriketi basi fanyeni hivyo msaidie kuwa sehemu ya mabadiliko kwenda kwenye maendeleo.


Angalia Serengeti Boys, sasa watu wanapambana kuisaidia kupata fedha. Hakuna hata benki, kampuni ya simu, kampuni ya vinywaji mfano Coca Cola, Pepsi, Serengeti, TBL na nyingine zilizo tayari kujitokeza. Wote kimya, lakini vijana wakienda kwa shida, wakafanya vizuri mtajitokeza siku ya kuwapokea!


Najua sihitaji kuwashawishi, lakini naamini ubunifu mdogo au matakwa binafsi ya maofisa masoko unazuia mengi katika udhamini katika michezo ili kusaidia mabadiliko kwenda kwenye maendeleo. Mbadilike.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic