April 17, 2017



Na Saleh Ally
PAMOJA na kwamba inaonekana suala la Simba kukata rufaa kwa Kagera Sugar wakipinga mchezaji Mohammed Fakhi kuchezeshwa akiwa na kadi tatu za njano limechukua sura kubwa ya ushabiki, lakini inawezekana ndiyo wakati ambao unadhihirisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linaweza likaendeshwa na upepo au matakwa ya watu binafsi na ushabiki pia.


Sikuwahi kulizungumzia hili sakata hata mara moja, tokea Simba wakiwa wamekata rufaa hadi waliposhinda rufaa yao na kupewa pointi tatu.


Lakini nilishangazwa na kuona suala hili linachukua sura kubwa, Kamati ya Saa 72 ikionekana kuyumba, Yanga wakionekana kulivalia njuga na wengi kujisahaulisha historia na rekodi hata za mwaka juzi, ikawa kama ndiyo mara ya kwanza timu imekata rufaa hapa Tanzania.


Sitaki kukumbusha kuwa Yanga walishinda rufaa wakapewa pointi tatu, misimu miwili iliyopota. Kumbuka Simba ilimchezesha Mussa Hassan Mgosi akiwa na kadi tatu za njano na Kagera Sugar ikashinda na kupewa pointi tatu na hii ikaisaidia Yanga kuwa bingwa.


Kuendelea kujadili ilikuwaje nyuma, kwangu naona si sawa kwa kuwa ni kitu kinachojulikana. Umekosea, umefanya uzembe unaadhibiwa. Sasa ushabiki uliotanda, unafanya suala hili liwe la kisiasa wakati ni kosa la kiufundi.


Kinachonishangaza, tunaona hata TFF na Bodi ya Ligi (TPLB), wanatuaminisha hawana uhakika wa rekodi za kadi zao, hii ni dhambi kubwa sana.


Nataka kujadili hili zaidi kuliko hiyo rufaa ya Simba. Ililazimika aitwe mwamuzi ili kupata uthibitisho kama kweli kadi imetoka. Simba walikata rufaa wakiwa na uhakika, TFF na Bodi ya Ligi walipaswa kuwa na uhakika zaidi kwa kuwa ndiyo watunza rekodi namba moja.


Kama kuna mkanganyiko wa rekodi ya kadi, dakika za mabao, wafungaji, bodi ya ligi na TFF ndiyo wanakuwa ni wenye uhakika zaidi kuliko mwingine yoyote. Sasa jiulize vipi Kamati ya Saa 72, ilihitaji kumuita mwamuzi na hakukuwa na hizo rekodi?


Lakini ajabu suala baada ya Kagera Sugar kupiga Simba kupokwa pointi zao, suala hilo limepelekwa kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ambayo ni kamati ya kutafsiri sheria.


Kamati hiyo inakwenda kuamua mkanganyiko wa kadi? Lakini safari hii ameitwa kocha wa kagera, ameitwa kiongozi wake na mchezaji Fakhi. Nao wataulizwa kama kuna kadi, unajua jibu lao litakuwa ni “Hapana”.


Kuna taarifa zinaeleza kuwa ameandaliwa Jonesia Rukyaa ambaye ni mwamuzi wa ligi kuu na alikuwa mwamuzi wa akiba siku hiyo aseme kwamba hakukuwa na kadi. Siamini Rukyaa anaweza kukubali kutumika kijinga hivyo.

Kama ni kweli akisema hivyo, mwamuzi ambaye alimpa kadi kasema ilikuwepo, bodi ya ligi inayotunza rekodi, imekubali ilikuwepo. Sasa Rukyaa anapinga kwa kipi?


Utaona siasa inachukua mkondo wake na kuonyesha kiasi gani haki inavyoweza kufinyangwa kwa matakwa. Au inaonyesha kiasi gani kweli hata bodi ya ligi au TFF haziwezi kuweka rekodi hata za kadi.


Nimeanza kuona shida kuanzia kwa uamuzi wa Simba, alilazimika mwamuzi kuitwa kuelezea. Akasema kweli alimpa kadi na kutoa vielelezo vyake. Kwa nini Bodi ya ligi au TFF wenyewe ndiyo wasingetumika kama watunza rekodi na kuthibitisha hilo.


Sasa anataka kutumika mwamuzi wa akiba kumpinga mwamuzi, ili aseme hapana na kuokoa mkoa anaotokea, kuokoa mkoa ambao Rais wa TFF, Jamal Malinzi yeye ni mwenyekiti wake.


Lakini jiulize? Kama uamuzi ulipitishwa Simba wapewe pointi, bodi ya ligi ambao ni sehemu ya watunza rekodi za ligi wakaandika barua kuitaarifu Simba kupewa pointi tatu. Kama ikitokea mwamuzi wa akiba akasema hakukuwa na kadi. Bodi ya ligi wataandika barua tena kusema pointi zimerudishwa Kagera?


Sitaki kuingia kwenye nani kapewa nani kapokonywa pointi. Lakini ninaendelea kupata hofu kubwa na uwezo wa viongozi wa TFF na bodi ya ligi! Tusubiri hiyo kesho.



1 COMMENTS:

  1. SAWA ALLY, nana hoja imebebwa kiushabiki kiasi cha watu kujitoa ufahamu, kwanza nina mashaka na barua yenyewe ya Kagera maana wameomba REVIEW na siyo APPEAL naamini hiyo Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji itaanzia hapo.........Kamati ya Masaa 72 iliundwa kikanuni na ile ya Sheria Kikatiba.....pili naanza kupata wasiwasi na mihemuko ya washabiki kuhusu hili suala na wengine wamefikia hata kusema Simba ilijuaje Fakhi ana kadi TATU ..........wanasahau kujiuliza Yanga walipokata Rufaa walijuaje Mgosi ana Kadi tatu...........tunaanza kufukua MAKABURI.........

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic